Wednesday, August 13, 2014

MAOMBI YA UTIMILIFU 5



Mwombaji wa Utimilifu

Wewe kama mwombaji wa maombi ya utimilifu yakupasa ufahamu mambo yafuatayo:
Omba Ukiwa katika Nafasi yako ya Mtoto wa Mungu
Unapomwendea Mungu kuomba maombi ya utimilifu nenda kama mtoto wake uliyekubaliwa naye, kwa njia ya Kristo Yesu.  Paulo alimwendea Mungu kama Baba, “…nampigia Baba magoti,” (Waefeso 3:14)  Fahamu ya kuwa Mungu Baba anakusikia kwa kuwa ni mtoto wake.
Omba Ukiwa na Ujasiri
Fahamu ya kuwa maombi ya utimilifu ni maombi yaliyo sawa na Neno la Mungu.  Neno lake ni mapenzi yake.  Kufahamu ya kuwa unaomba kama Mungu atakavyo yaani unapo omba katika mapenzi yake, unakuwa na ujasiri wa imani katika kupokea, “Na huu ndio ujasiri tulionao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia.” (1 Yohana 5:14).  Kwa upande mwingine ujasiri wetu mbele zake katika maombi unatokana na maisha ya kumpendeza tunayoishi mbele zake. Haya ni maisha ya kulitenda Neno lake, maandiko yanasema,”Wapenzi, mioyo yetu isipotuhukumu, tuna ujasiri kwa Mungu; na lo lote tuombalo, twalipokea kwake, kwa kuwa twazishika amri zake, na kuyatenda yapendezayo machoni pake” (Yohana 3:21-22).
Omba kwa Bidii
Omba kwa kumaanisha, usitamke maneno matupu mbele za Mungu, sema maneno yaliyoushika moyo wako, ambayo yako sawa na Neno la Mungu.  Omba kwa kung’ang’ania, usiwe mwepesi kuondoka mbele za Mungu.  Maombi yako usemayo mbele zake yawe kama ni uhai wako mwenyewe, yaani kama sehemu ya maisha yako.  Maombi ya namna hii ni maombi ya bidii, mara nyingine maombi haya huambatana na machozi au kufunga, ukiyafanya kama mtu mwenye haki utapokea, “…Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa bidii.” (Yakobo 5:16).
Omba kwa Jina la Yesu
Omba kwa kutumia Jina la Yesu, omba kwa kibali na mamlaka aliyokupa Yesu mbele za Baba, yaani Jina lake, “…Mkimwomba Baba neno lolote atawapa kwa jina langu.” (Yohana 16:23).  Tegemea kuona matokeo katika maisha yako na Kanisa baada ya kuanza kufanya maombi na maombezi ya utimilifu.

Sentesi zifuatazo zinaonyesha kwa kifupi maombi ya utimilifu:

Baba kwa jina la Yesu ninaomba unisimamishe imara katika mapenzi yako yote, Nifanye imara moyo wangu niweze kutenda mema katika utimilifu wote yaani, nisifanye lolote lililo baya.  Nguvu za Roho Mtakatifu ziambatane nami wakati wote katika huduma. Ninakuomba Baba pendo lako ndani yangu lizidi katika hekima yote na ufahamu wa rohoni.  Pia ninaomba haya kwa kanisa lako na watumishi wako wote, ili watimilike katika kutenda mapenzi yako, kutenda mema,katika nguvu zako na katika pendo linalotuunganisha na kutupa umoja.  Kwa jina la Yesu, Amina.

 Ikiwa kitabu hiki kimekupa hatua mpya au una swali lolote usisite kuwasiliana nami kwa anuani na simu zilizopo mwanzoni mwa kitabu.  Pia ni vizuri kama utaweza kupata vitabu vingine ambavyo nimeviandika kwa msaada wa Mungu ili ujengwe kiroho.

Ikiwa unapenda kuwa mwombaji na kuombea utimilifu lakini bado haujampa Yesu Maisha yako sema sala Hii:

Mungu Baba ninkuja kwako kwa jina la Yesu, naomba unisamehe dhambi zangu.  Yesu Mwokozi ingia ndani yangu, uwe Bwana na Mokozi wangu, naamini ulikufa na kufufuka, ili kwa damu yako nitakaswe na kuhesabiwa haki, nisiingie katika hukumu ya Mungu.  Ninakushukuru Baba kwa jina la Yesu, Amina.

No comments:

Post a Comment