Monday, August 11, 2014

Maombi ya Utimilifu 3




Utimilifu Katika Kutenda Mema

Wakati fulani nilipewa maneno yafuatayo moyoni mwangu, “Iweni na juhudi katika kutenda mema, maana wakati wenu ni mchache”.  Kwa maneno haya nilipata msisitizo kwamba kutenda mema ni jambo la muhimu sana tunapokuwa hai.

Paulo aliwaombea Wakorintho wasitende mabaya alisema, “Nasi twamwomba Mungu, msifanye lolote lililo baya(2 Wakorintho 13:7).  Bila shaka Mungu alijibu maombi haya kwa kuwapa neema Wakorintho ya kutotenda mabaya kwa msaada wa Roho wake. 

Kutenda Mema na Neno la Mungu

 Mungu hutuwezesha kutenda mema kwa njia ya Roho Mtakatifu katika Neno lake.  Roho wa Mungu huyahuisha maandiko ndani yetu na hivyo yakawa ni Maneno ya Mungu yenye pumzi yake.  Neno la Mungu katika Roho Mtakatifu linaweza kumkamilisha mtu katika kila tendo jema.  Jinsi unavyokuwa na bidii ya kulijua Neno na kupata ufahamu wa Roho kupitia Neno, ndipo unapozidi kukamilika katika kutenda mema. Unaposikiliza Neno, omba uweze kulielewa na kujua linakuonya kitu gani, linakuongoza ufanye nini, na linakuandaaje kutenda haki.  

Ukijizoeza kufanya hivi matendo mema yatakuwa ni sehemu ya maisha yako, kwa nguvu ya Neno la Mungu lililo hai.  Maandiko yanasema, “Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema
(2 Timitheo 3:16-17).   Hivyo fanya maombi kwaajili yako na maombezi kwa wengine wakamilishwe katika kutenda mema kwa njia ya kukutana na Neno lenye pumzi ya Mungu.  Uwaombee watu wote unaowafahamu ambao husema Neno; yaani wanaofundisha, wanaohubiri nk. Omba waweze kusema Neno lenye pumzi ya Mungu, liwezalo kuwabadidilisha wanaosikia na kuwafanya wakamilike katika
kutenda mema. 
Matendo Mema ni Nuru
Utimilifu katika kutenda mema unatukamilisha katika kazi yetu ya kuwa nuru ya ulimwengu.  Sisi kama watu wenye Nuru (Yesu) twaangaza duniani kwa matendo mema ya Yesu akaaye ndani yetu. Matendo mema ni nuru.   Maandiko yanasema, “Ninyi ni nuru ya Ulimwengu.  Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima.  Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani.  Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele za watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.” (Mathayo 5:14-16).  Wakati wote nuru ing’aapo giza haliwezi kushinda,  Nayo nuru yang’aa gizani, wala giza halikuiweza”(Yohana 1:5). Ubaya (giza) hauwezi kushinda tutendapo mema(nuru). Hii ndio maana Biblia inatuagiza, kwa kusema, ”usishindwe na ubaya(giza), bali uushinde ubaya kwa wema(nuru).” (Warumi 12:21).  Kuombea utimilifu katika kutenda mema kutatuwezesha kuangaza kwa matendo hayo, hatimaye watu watamwinua/watamtukuza Mungu, wayaonapo matendo yetu mema.

Kutenda Mema ni Mbegu

Kama mkulima asivyochoka kupanda mbegu, kwa kuwa anatarajia mavuno kwa wakati wake ndivyo itupasavyo kufanya.  Matendo mema kwa wanaotuudhi, walioamini na watu wote ni mbegu, maandiko yanasema, “Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho.  Kwahiyo kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema; na hasa jamaa ya waaminio.” (Wagalatia 6:9-10).  Utendapo mema kwa wanadamu Bwana atayahifadhi matendo hayo mbele zake kama mbegu na kukupa mavuno.  Kornelio alitenda mema na Mungu akayahifadhi matendo yake kama mbegu, baadae alimpa mavuno, yaani malaika kumtokea na kusema naye
(Matendo 10:1-8).

 Upandapo mema utavuna mema, maombi ya utimilifu katika kutenda mema yatakuwezesha kupanda mema.  Unapomgawia mwenye njaa chakula, aliye uchi mavazi na kufanya maombezi, Bwana hatasahau matendo hayo mema, atakulipa kama yasemavyo maandiko, “mkijua ya kuwa kila neno jema alitendalo mtu atapewa lilohilo na Bwana…(Waefeso 6:8). 

Kufanywa Imara Katika Kutenda Mema

Mungu hutoa neema ya kutotenda mabaya kwa njia ya kumfanya  mtu imara katika kila neno na tendo jema, “…Mungu Baba…awafariji mioyo yenu, na kuwafanya imara katika kila neno na tendo jema
(2 Wathesalonilke 2:16-17). Kutenda mema wakati unafanyiwa mabaya si kitu rahisi, kumsema mtu vizuri au kumfanyia kitu kizuri wakati yeye anakufanyia kitu kibaya si jambo rahisi kwa mtu wa kawaida.  Maandiko yanasema, “…Wapendeni adui zenu, watendeeni mema wale ambao wawachukia ninyi…msimlipe mtu ovu kwa ovu. Angalieni yaliyo mema machoni pa watu wote…Maana huu ndio wema hasa  mtu akivumilia huzuni kwa kumkumbuka Mungu, pale ateswapo isivyo haki (Luka 6:27, Warumi 12:17). 

Mtu yoyote aliye na Yesu yampasa kuwatendea mema watu wote wabaya kwa wema. Ili kuweza kutenda mema kwa watu wote wakiwemo wanaokuchukia inakupasa uwe imara kiroho, maana si jambo rahisi.  Ili kutenda tendo jema kama vile kumuombea, kumvisha, kumsalimu, au kumpa zawadi mtu, yakupasa uwe umetiwa nguvu katika Roho Mtakatifu kuyatenda hayo.

Ili kufanywa imara na kutimilika katika kutenda mema kwa watu wote, yakupasa uombe Mungu akusaidie na uwaombee wengine pia.  Ni vizuri kuwaombea watumishi wa Mungu au washirika katika kanisa lako, wasifanye lolote lililo baya.  Kisha unaweza kuendelea kuwaombea wafanywe imara au watiwe nguvu katika kutenda mema.  Ukifanya hivi utakuwa unawasaidia kufanana kitabia na Yesu ambaye,“… alipotukanwa, hakurudisha matukano; alipoteswa hakuogofya…” (1 Petro 2:23). 

Inawezekana  kuwa umekutana na mtu asemaye kulipiza kisasi ni sawa au haiwezekani kusamehe.  Mtu wa namna hii yampasa aombewe utimilifu katika kutenda mema kwa njia ya kufanywa imara katika kutenda mema, yaani afanywe imara ili aweze kusamehe au kutolipiza kisasi.

Kutenda Mema na Hekima

Kutenda mema kuna uhusiano wa karibu na hekima ya Mungu.  Mtu mwenye hekima hufanya mambo mazuri hutenda mema na ana matunda mema. Maandiko yanasema, “N’nani aliye na hekima na ufahamu kwenu? Na aonyeshe kazi zake kwa mwenendo wake mzuri, katika upole wa hekima…Lakini hekima itokayo juu kwanza ni safi, tena ni ya amani, ya upole, tayari kusikiliza maneno ya watu, imejaa rehema na matunda mema, haina fitina, haina unafiki.” (Yakobo 3:13,17).  Mambo yaliyotajwa hapa ni matendo ya hekima itokayo juu, haya ni matendo mema.  Kuwa na amani na watu ni tendo jema la hekima, kuwa mpole/kutolipiza kisasi ni tendo jema la hekima, kusikiliza watu, kutokuwa mnafiki, kutofitini haya yote ni matendo mema ya hekima.

Ikiwa tumepungukiwa matendo haya inawezekana tumepungukiwa na hekima ya Mungu itokayo juu, maana inayo matendo hayo mema.  Kama tumepungukiwa na hekima twaweza kuomba, “Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu, awapaye wote kwa ukarimu, wala hakemei; naye atapewa.” (Yakobo 1:5). 

Namna nyingine ya kuombea utimilifu katika kutenda mema ni kuomba hekima ya Mungu iongezeke katika maisha yetu, katika Kanisa na watumishi wa Mungu.  Hekima ya Mungu mioyoni mwetu itatuelekeza jinsi ya kufanya au kusema pale tunapokutana na mazingira yanayoweza kusababisha tutende mabaya.  Hekima hii itatuokoa kwa kutupa njia au mlango maalum wa kutenda mema, mahali ambapo kwa hali ya kawaida tungetenda mabaya. Kwa mfano, wakati wa kulaumu au kukasirika hekima itatufundisha katika mioyo kutokasirika. 
Usiache wala kuchoka kuombea utimilifu katika kutenda mema, kwa njia ya kuombea ongezeko la hekima ya Mungu ndani ya Mwili wa Kristo/Kanisa.

No comments:

Post a Comment