Utimilifu
Katika Mapenzi ya Mungu
Mapenzi ya Mungu ni utashi wake, ni namna anavyotaka
tuishi. Bila kutimilika katika kuyafanya
mapenzi yake hakuna mtu awezaye kumwona,
“si kila mtu aniambiaye Bwana,
Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya
Baba yangu aliye mbinguni” (Mathayo 7:21). Hivyo kufanya mapenzi ya
Mungu ni kitu cha muhimu sana kwa watu wake, wanaotarajia kumuona.
Maombezi Wasipungue katika
Kumpendeza
Mapenzi ya Mungu twaweza kuyafanya kwa njia ya
kuwezeshwa na neema yake. Neema hii ipo
ndani ya Neno lake ambalo ni mapenzi yake (Mathayo 12:50, Luka 8:21). Kitu
kingine kinachoweza kutusaidia kufanya mapenzi yake ni maombi na maombezi ya
utimilifu katika kuyafanya. Katika
baadhi ya maandiko yaliyopita tulimwona Epafra akiwaombea Wakolosai kwa bidii ili wasimame wakamilifu na
kuthibitika sana katika mapenzi yote ya Mungu.
Hapa aliwaombea wasipungue katika kumpendeza Mungu.
Kupingana Nguvu za Giza
Tarehe 12.6.2006, wakati ninaomba asubuhi, ndani yangu nilipata ufahamu
ya kwamba kuna aina ya pepo na wakuu wa giza ambao wanapinga na kujaribu kuzuia
maandeleo ya mtu kukua kiroho na kufanya mapenzi ya Mungu. Pepo hawa humfuatilia kila mtu aliyempa Yesu
maisha yake, hata kujaribu kumzuia asisonge mbele kwa njia ya kuleta hali
mbalimbali za kumpinga. Hali hizi ni
kama vile, kumpa mawazo ya kutosoma Biblia, kutoenda katika ibada au kuchochea
utendaji wa utu wa kale kwa njia ya kuleta mawazo machafu.
Inawezekana kabisa Paulo alipoandika, “Lakini nachelea; kama yule
nyoka alivyomdanganya Hawa kwa hila yake, asije akawaharibu fikra zenu, mkauacha
unyofu na usafi kwa Kristo” (2Wakorintho 11:3), moyoni mwake alijua ya
kuwa Shetani, wakuu wa giza na mapepo wanafuatilia watu walio okoka. Sababu ya Shetani kufanya hivyo ni ili waache
unyofu na usafi, yaani wasimpendeze Mungu.
Bila shaka Epafra alipowaombea Wakolosai kwa bidii na kwa kushindana
alikuwa anapambana na pepo waliojaribu kuwazuia wasikue kiroho na kufanya
mapenzi ya Mungu. Paulo alipoandika, “Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu
wa giza hili, juu ya jeshi la pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.”(Waefeso 6:12). Alitumia
neno “kushindana”
lililofanana na jinsi alivyoomba Epafra, yaani kuomba kwa bidii. Hivyo twaweza kusema, Epafra alipoomba kwa bidii ili
wathibitike katika mapenzi yote ya Mungu kwa sehemu alikuwa anashindana na
nguvu za giza zilizojaribu kuwazuia kufanya ayatakayo Mungu. Nguvu hizi ni zilezile ambazo Yesu
alizishinda kwaajili yetu na kuzifanya si kitu (Wakolosai 2:15). Wakuu hawa wa giza na mapepo hawawezi kutenda
lolote wakikutana na mamlaka ya Yesu kupitia mtu afanyaye maombezi kwa jina la
Yesu. Kwa hiyo Epafra aliposhindana nazo
alikuwa upande wa ushindi kwa kuwa alikuwa na Jina hilo akiwa ndani ya Kristo
Yesu aliyeshinda.
Maombi ya Kujua Mapenzi ya Mungu
Paulo aliwaandikia Warumi maneno yafuatayo, “Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali
mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate
kujua hakika mapenzi ya Mungu
yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.”
(Warumi 12:2). Mapenzi ya Mungu ni mema
na ukamilifu. Kuyajua kunaweza kukuwezesha
kuyatenda na kuwa mkamilifu. Baada ya
nia (fikra/mawazo) kufanywa upya kwa Neno la Mungu, utaweza kuyajua mapenzi ya
Mungu kwa upana na kuzidi kukamilishwa.
Paulo aliwaombea Waefeso macho ya mioyo
(roho,fikra, mawazo, nia) yatiwe nuru ili wajue
(Waefeso 1:18). Wewe pia endelea,
kujiombea, kuombea watumishi, na kuliombea Kanisa liendelee kuyajua mapenzi ya Mungu kwa kutiwa
nuru katika nia. Matokeo yatakuwa kulijua Neno la Mungu, kufanywa upya, na
hatimaye kuweza kulitenda. Hali hii italiwezesha Kanisa kufikia utimilifu wa
kufanana na Yesu katika kutenda mapenzi ya Mungu. Usichoke kufanya maombi haya, muombe Mungu
akuwezeshe kutenda mapenzi yake yote. Mueleze ya kuwa kwa nguvu zako huwezi lakini kwa neema yake
inawezekana. Baada ya hapo ombea Kanisa
taja mtu unayeweza kumkumbuka, ili aweze kuthibitika
katika mapenzi ya Mungu. Kisha ombea
watumishi wa Mungu wale unaowajua na usiowajua waweze kuthibitika katika
mapenzi yote ya Mungu.
Ikiwa wewe ni Mchungaji wa kweli, Mwinjilisti wa
kweli, Mwalimu wa kweli, Nabii wa kweli, Mtume wa kweli, Mwombezi au kiongozi yoyote
ambaye watu wanakutegemea. Usiache kuwaombea watimilike katika kuyafanya
mapenzi ya Mungu. Matunda ya kazi yako
kwao yanategemeana sana na mwisho wao, ambao pia unategemea ni jinsi gani
walimpendeza Mungu.
No comments:
Post a Comment