Saturday, August 9, 2014

Maombi ya Utimilifu 1



Waombee Unaowahudumia

Tarehe 31.1.2006, Roho wa Mungu aliniongoza moyo wangu kwa maneno haya “Waombee unaowahudumia, angalia mfano wa Paulo”.  Baada ya kupata ufahamu huu, nikagundua ya kuwa mtume Paulo aliwaombea sana watu aliowahudumia, pia alihitaji maombi kutoka kwao.

Baada ya muda mfupi nilipata mawazo ya kufundisha somo ambalo litaonyesha ni jinsi gani kanisa la kwanza waliomba na waliwaombea watumishi, pia jinsi gani watumishi waliwaombea waumini.  Kati ya Maombi ambayo niliyaona katika maandiko, waliyoyaomba watumishi hawa,  yalikuwa ni ‘maombi ya utimilifu’.  Haya ni maombi yaliyoombwa kwaajili ya mtu ambaye tayari amempa Yesu maisha yake. 

Kwa wakati wa sasa  ni maombi ambayo Mchungaji, Mwinjilisti, Mmishionari, Mwalimu, Shemasi au mtumishi mwingine yoyote wa Mungu anaweza kuwaombea watu anaowahudumia.  Kwa upande mwingine maombi haya yanaweza kuombwa na watu wanaoipokea huduma hiyo, yaani kuwaombea wanaotoa huduma kwao.

Twaomba Kutimilika Kwenu

Paulo aliwaandikia Wakorintho, “Maana twafurahi, iwapo sisi tu dhaifu, nanyi mmekuwa hodari. Tena twaomba hili nalo kutimilika kwenu
(2 Wakorintho 13:9).  Pamoja na kuuona uhodari wao kama yasemavyo maandiko haya, Paulo aliona hiyo bado haitoshi na hivyo kuongeza maombi ya utimilifu kwao.  Mahali pengine aliandika, “Hatimaye ndugu kwaherini; mtimilike…”  (2 Wakorintho 13:11).  Maombi na matamshi ya mtumishi huyu wa Mungu kuhusu kutimilika aliyafanya kwa watu aliowahudumia.

Katika kitabu cha Wakolosai 4:12, Paulo alimuelezea Epafra kama ifuatavyo, “Epafra , aliye mtu wa kwenu, mtumwa wa Yesu Kristo awasalimu akifanya bidii (bidii hapa ni hali ya kumaanisha katika moyo, ni hali ya kuomba kwa mfano wa mtu apiganaye mieleka) siku zote kwaajili yenu katika maombi yake ili kwamba msimame wakamilifu na kuthibitika (kusimama) katika mapenzi yote ya Mungu

Katika maandiko haya yote Paulo alitumia neno Kutimilika au Wakamilifu akiwa na maana ya; (i) Kuwa kamili (ii) Kurejeshwa na (iii) Kukua katika tabia ya Kristo.  Maahali pengine kuhusiana na kukua katika tabia ya Kristo aliandika, “vitoto vyangu, ambao kwamba nawaonea utungu tena mpaka Kristo aumbike ndani yenu” (Wagalatia 4:19).  Kwa maneno mengine katika maandiko haya Paulo alikuwa anasema, “ Vitoto vyangu, ambao kwamba nawaonea utungu katika maombi yangu kama mwanamke aliye karibu na kujifungua, nafanya hivyo mpaka tabia ya Yesu iumbike ndani yenu, yaani izaliwe ndani yenu ili mtimilike

Maombi waliyoomba Paulo na Epafra kuhusu utimilifu yalikuwa sawa na Yesu alivyosema alisema, “Basi ninyi mtakuwa wakamilifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu”(Mathayo 5:48).  Neno hili “Wakamilifu” limefanana na “Watimilifu” katika lugha ya Kiyunani.  Ukamilifu aliousema Yesu hapa unahusiana na kufanana na Mungu kitabia, hasa wema wake, kama vile kuwatendea mema wote wabaya kwa wema.

Kama vile watumishi tuliowasoma kwenye maandiko walivyofanya maombi ya kuombea utimilifu, sisi pia tunaweza kujiombea wenyewe na kuombea wengine, hasa wale tunaowahudumia.  Kuna maeneo kadhaa ya ukamilifu/utimilifu ambayo tunaweza kuyaombea katika maisha ya mtu, Tutayaangalia maeneo haya toleo linalofuata.









No comments:

Post a Comment