Friday, August 1, 2014

Kazi Njema za Ulimi



Kazi Njema

Pamoja na kutaja baadhi ya kazi mbaya za ulimi, pia Kuna kazi njema.  Mungu alipomuumba mtu alimuumba mkamilifu asiye na shida baada ya anguko ulimi ulipata shida.
Kutenda Kazi na Mungu
Mungu ameweka ulimi katika viungo vya mwanadamu kama chombo cha kumiliki na kutawala.  Biblia inasema “Adamu akawapa majina yao kila mnyama wa kufugwa na ndege wa angani na kila mnyama wa mwituni”(Mwanzo 2 : 20).  Msitari wa kumi na tisa unaonyesha kila jina alililoita wanyama ndilo lilikuwa jina la wanyama hao.  Hii inaonyesha kwa sehemu Adamu alikuwa na mamlaka ya kusema kitu na kikawa.  Mungu alimuumba Adamu na alimshirikisha kutenda kazi pamoja na yeye. Mungu  alimshirikisha kazi yake kwa njia ya kutoa majina kwa ulimi .  Sasa kwa njia ya Yesu Kristo tunao uweza ule ule wa kumiliki  kwa njia ya Neno lake tuliwekalo mioyoni mwetu.  Kwa ulimi tutaweza kuwa watenda kazi na Mungu kwa Neno lake.  Mungu aliumba vitu vyote baadaye akashirikiana na Adamu  kuwapa majina kwa ulimi wake.  Sasa amemtoa Yesu na anashirikiana nasi kutenda kazi yake ametupa huduma ya upatanisho kwa neno la upatanisho katika vinywa vyetu (2 Wakorintho 5 : 19). Kwa njia ya ulimi tunatenda kazi na Mungu kwa Neno kale, “Nao wale wakatoka, wakahubiri kote kote, Bwana akitenda kazi pamoja nao, na kulithibitisha lile neno kwa ishara zilizofuatana nalo.” (Marko 16:20). Bwana alilithibitisha Neno walilolihubiri mitume kupitia ndimi zao.  Kwa ulimi waliunganishwa na ulimwengu wa miujiza kwa Neno la Mungu.  Hilo linatokea hata kwetu, tunapojaza neno mioyoni na kulisema kwa ufunuo wa Roho. Mungu huanza kutenda kazi na sisi hii ni kazi njema ya ulimi. 
Pia kwa njia ya maombi mapenzi ya Mungu hutimia duniani kama mbinguni, kwa njia ya ulimi maombi haya hutendeka. Ulimi mmoja unaweza kubadilisha  ukoo, nchi na hata dunia kwa njia ya maombi.  Mungu anapotaka kutenda mapenzi yake duniani huliweka neno lake kinywani  mwa mtu.

Kutakaswa
Kwa njia ya ulimi tunatubu na kutakaswa dhambi zetu.  Kwa njia ya ulimi uhusiano wetu na Mungu unarejeshwa kwa toba na utakaso wa dhambi kupitia damu ya Yesu.  Unaweza kusoma (1Yohana 1:9). Katika kitabu cha Warumi imeandikwa, “Wala msiendelee kuvitoa  viungo vyenu kuwa silaha za dhuluma kwa dhambi, bali jitoeni wenyewe kwa Mungu kama walio hai baada ya kufa, na viungo vyenu kwa Mungu kuwa silaha za haki,”(Warumi 6 :13).  Msitari wa kumi na tisa unasema “…kwa kuwa kama mlivyovitoa viungo vyenu vitumiwe na uchafu na uasi mpate kuasi, vivyo hivyo sasa vitoeni viungo vyenu vitumiwe na haki mpate kutakaswa.” Ndimi zetu zinapotumiwa na haki huleta utakaso katika maisha.  Hii hutokea ndimi zetu zinapokuwa chombo cha Neno la Mungu maana Neno hutakasa. Tuliona mwanzoni yatokayo moyoni humtia mtu unajisi.  Lakini pia yatokayo moyoni, moyo ulio na Neno la Mungu hutakasa, ulimi unatia unajisi ikiwa moyo hauna Neno, lakini pia unayo kazi ya kutakasa kwa Neno.

Kutukuza
Biblia haituonyeshi moja kwa moja kama Adamu aliutumia ulimi wake kumtukuza Mungu. Mimi ninaamini alipoumbwa aliishangaa uumbaji ambao Mungu aliufanya kabla hajamuumba.  Inawezekana kabisa baada ya kuushangaa alimwinua na kumtukuza kwa ulimi wake.  Tutangalia sehemu mbili katika maandiko ambazo zinaonyesha kazi ya ulimi ni kumtukuza Mungu.  Unaposoma maandiko haya angalia sehemu nilizokoleza na uzifananishe utajifunza vizuri zaidi. “Nimemweka BWANA mbele yangu daima, kwa kuwa yuko kuumeni kwangu, sitaondoshwa.  Kwa hiyo moyo wangu unafurahi nao utukufu wangu  unashangilia….”(Zaburi 16:8-9). “….Nalimwona Bwana mbele yangu sikuzote, kwa kuwa yuko upande wa mkono wangu wa kuume nisitikisike.  Kwa hiyo moyo wangu ukapendezwa Ulimi wangu ukafurahi;” (Matendo 2 : 25-26) kwa maandiko haya mawili tunaweza kusema ulimi wa mtu ni utukufu wake.  Ulimi wa mtu ni chombo cha utukufu wa Mungu.  Hii ilionekana wakati wa siku ya Pentekoste walipojazwa Roho Mtakatifu walisikiwa wakitumia ndimi zao kumtukuza Mungu. “Wakrete na Waarabu; tunawasikwa hawa wakisema kwa lugha zetu matendo makuu ya Mungu” (Matendo ya Mitume 2 : 11).  Ndimi zetu zimeumbiwa utukufu wa Mungu.  Shetani anataka sana kuharibu jinsi, tunavyoongea kwa kuwa mara zote hupenda kutumia visivyo (mis-use) vitu vya Mungu.  Neno lolote ambalo halimpi Mungu utukufu, litokapo katika vinywa vyetu, hutufanya kuutumia ulimi pasipo makusudi yake. Katika kitabu cha Wakolosia imeandikwa “Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye”(Wakolosai 3:17).  Maneno tusemayo ambayo yanaleta msukumo kwa tuyatendayo inapasa yawe kwa utukufu wa Mungu.  Maneno inapasa yaonyeshe kumwinua na kumtukuza Mungu hiki ni moja ya kipimo cha maneno yetu. Je yanampendeza Mungu? Kama yanampendeza basi yanamtukuza.  Kazi ya ulimi ni kumtukuza. 

Kukiri
Yesu ni kichwa cha Kanisa ni kuhani wetu mkuu mbele za Mungu. Amekwenda mbinguni kwaajili yetu, yupo mkono wa kuume wa Mungu kwaajili yetu.  Je, tunaunganishwa naye kwa jinsi gani? Ni kwa maungano yetu.  Biblia inasema, “ Kwa hiyo, ndugu watakatifu, wenye kuushiriki mwito wa mbinguni, mtafakarini sana mtume na kuhani mkuu wa maungano yetu, Yesu,”(Waebrania 3 : 1).
Jinsi tunavyoongea duniani kama vile neno lisemavyo tuna ‘m-keep bize’ Yesu mbinguni.  Tunampa matirio yaani  maneno ya kuyafanyia kazi kama kuhani. Kukiri ni kusema kama Mungu asemavyo katika maandiko.  
Tunasema kama Neno lisemavyo, tunasema Yesu alitufanyia nini msalabani, alipofufuka na alipoketi mkono wa kuume.  Tunasema sisi ni nani kwake, yeye ni nani kwetu, tunasema kama Neno lisamavyo.  Imani ya Neno la Mungu huanzia mioyoni mwetu na utimilika vinywani mwetu. Imani hii iwapo kinywani kwa njia ya maneno tusemayo humwingiza Yesu kazini. Yesu amepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.  Anapata nafasi duniani kwa maneno yetu yaliyosawa na Neno lake.  Tunapotamka maneno haya, mamlaka ya utendaji wake hujidhihirisha. Biblia inasema, “Basi iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia  katika mbingu, Yesu mwana wa Mungu na tuyashike sana maungano yetu,” (Waebrania 4 :14). Tunayashika maungano yetu, yaani maneno yetu yalisemalo Neno lake maana ameingia katika mbingu kwaajili yetu, ayahudumie maungano yetu.

Wakati  fulani nilipompa Yesu maisha yangu mwezi wa kumi mwaka 1989 moyoni mwangu nilipata ushuhuda usemao “Amini usemayo”.  Yalikuwa ni maneno yaliyojirudiarudia ndani yangu. Siku moja nilikutana andiko linalofana na mawazo hayo linasema,  Lakini kwa kuwa tuna roho ile ile ya imani kama ilivyoandikwa, naliamini na kwasababu hiyo nalinena;    sisi nasi twaamini na  kwasababu hiyo twanena”(2Wakorintho 4:13).  Imani iliyopo moyoni husema kinywani.  Kile unachokijua kuhusu Mungu, kuhusu wewe katika Mungu au ushindi wako katika Kristo utakisema kwa kinywa chako, pia utakitarajia kudhihirika kwa kuwa unaye kuhani aliyesimama mbinguni kwaajili yako, ili adhihirishe maungano au maneno yako ya imani.







No comments:

Post a Comment