Maandiko matakatifu yanaonyesha
kwamba malaika wa Mungu wapo na wanatenda kazi pamoja na watu wa Mungu; katika
kuwahudumia na vita vya kiroho. Kwa
mfano hebu soma maandiko haya, “Malaika
wa BWANA hufanya kituo, akiwazunguka wamchao na kuwaokoa” (Zaburi 34:7), “Waaibishwe wafedheheshwe, Wanaoitafuta nafsi
yangu. Warudishwe nyuma,
wafadhaishwe…Wawe kama makapi mbele ya upepo, Malaika wa BWANA akiwaangusha
chini.” (Zaburi 35:4-5), “Kwa kuwa
atakuagizia malaika zake Wakulinde katika njia zako zote.” (Zaburi 91:11).
Katika makabiliano ya vita vya kiroho, malaika wa Mungu wanatenda kazi hata
sasa, ikiwa tunawaona au ikiwa hatuwaoni.
Mama Mbise amepewa neema ya kuona utendaji wa malaika wakati akiwa
katika mapambano ya kiroho katika huduma.
Karibu usome shuhuda hizi tena:
Wakati fulani mgonjwa aliletwa nyumbani kwangu ili
aombewe. Alikuwa ni ndugu wa rafiki zetu
huko Njani. Alitokea hospitali ya
KCMC. Alikaa siku tatu wakati huo huo
tukiendelea na maombi. Vita vilikuwa
vikali sana
alikuwa hawezi kuongea mdomo umepinda nk.
Baada ya siku nne alianza kupata ufahamu. Baada ya wiki moja alianza kukaa na kufanya
mazoezi ya kutembea. Tulikuwa na dada
aliyekuwa akitusaidia kazi aitwaye Esta aliokea Nkwanekoli. Siku moja saa tano mchana wakati Esta anamwogesha mgonjwa, mimi
nilikuwa chumbani naomba. Baada ya
kumaliza maombi nikakaa kitandani, ghafla upepo ukaanza kuingia chumbani kwa
mfano wa moshi, ulikuwa wa rangi kama ya
kijivu au bluu. Ulikuwa ni mfano wa
ukungu mzito. Nikaanza kushindwa kupumua. Nikaanza kuomba na kukemea. Ghafla ndani ya ule moshi nikaona viumbe
vingii!, kama viwatu vidogo vidogo. Mwonekano wake ulikuwa kama
askari wengi wenye mavazi ya kivita, walikuwa wameshika vitu mfano wa virungu (Maandiko yanasema vita vyetu vinahusika na jeshi la pepo wabaya
katika ulimwengu wa roho, inawezekana hawa walikuwa ni moja ya kikosi cha pepo
hao- Waefeso 6:12). Walianza kunipiga na mimi niliendelea kukemea, nikaona kama vile ninazidiwa nguvu nikalegea wakachukua miguu
yangu na kuiweka kitandani. Yakatokea
majitu mengine makubwa mawili, walikuwa na maumbo kama
watu lakini hawakuwa watu! (Inawezekana hawa ni wakuu wa giza ambao walikuwa ni majemedari wa jeshi la
pepo hawa).
Wakachukua kamba kubwa wakaiviringisha na kunifunga mpaka
kwenye mabega yangu. Wakaanza kunibeba
na kusema “Dawa yake huyu ni kumbeba na kumpeleka, ni kumtowesha asionekane
tena” Nikajiona natoka kitandani mpaka
pua yangu ikagusa dari. Ghafla nilisikia
sauti ya kishindo kama radi “PAAA” Wakatokea
malaika wawili wakubwa!! Mmoja akasimama kushoto kwangu na mwingine kulia. Kila mmoja ameshika upanga, ambao ulikuwa ni kama moto uwakao!! Sikujua wameshikaje mapanga yale maana
mpini ulikuwa hauonekani ilikuwa kana kwamba wameshika kwenye moto. Malaika hawa walikuwa wana utisho mkuu. Walikuwa wazuri wenye sura za huruma zenye
kung’aa, pia walikuwa na mabawa makubwa yaliyovuka mabegani mwao. Urefu wao haukupungua futi saba au nane hivi. Mmoja wao akasema, “hapo hapo asitoke hata
mmoja” Akafunua chini kwa mfano wa mtu
afunuaye mfuniko wa shimo la maji
machafu. Wale malaika wakawaambia,
“Hamna mamlaka huyu ni mtumishi wa Mungu, amekombolewa na damu ya Yesu”. Wakachomoa kitu mfano wa kadi za benki au
kadi ya ATM, kilikuwa cha rangi nyekundu wakawaonyesha na kusema, “Huu ndio
ushahidi”, Halafu wakasema, “Mko wangapi?” wakajibu, “Elfu moja mia sita” ,
Malaika akasema, “Kuanzia sasa hamtafanya kazi tena duniani” Halafu
wakawatumbukiza ndani ya lile shimo kwa kuwaamrisha.
Wakati huo nilikuwa kitandani nimefungwa kamba, Dada Esta
akafungua mlango alikuja kuchukua mafuta ya kumpaka mgonjwa, akaanguka chini na
kuanza kunena kwa lugha muda mrefu.
Alipokuwa akinena kamba niliyokuwa nimefungwa ikaanza kulegea. Alipomaliza kunena tu, kamba zote zilikuwa
zimeniachia (Kunena kwa lugha za Roho Mtakatifu
kunaweza kumfungua mtu na kamba za kishetani zinazoonekana na zisizo onekana,
usiache kunena kwa lugha. Mfano huo
tumeuona kwa dada Esta). Wakati huo malaika walikuwa
wameshaondoka. Baadaye Esta aliniambia
alipofungua mlango aliona watu wanaongaa sana
na akashindwa kustahimili na kuanguka.
No comments:
Post a Comment