Saturday, August 30, 2014

Fahamu ya Kuwa Mungu Habadiliki


Fahamu ya Kuwa Mungu Habadiliki

Ni vizuri kumfahamu Mungu huwa ana tabia gani katika utendaji wake, ili upokee mahitaji yako.

Mungu Habadiliki

Mungu uliyenaye ni Mungu asiyebadilika, ni Mungu asiye na kigeugeu. Maandiko yanasema, “Mungu si mtu, aseme uongo; Wala si mwanadamu, ajute (abadilishe nia au mawazo yake); (Hesabu 23:19). Mungu hageuki geuki na kubadilika kama watu wafanyavyo. Andiko lingine linasema, “Kwa kuwa mimi, BWANA, sina kigeugeu; ndio maana ninyi hamkuangamizwa, enyi wana wa Yakobo. (Malaki 3:6). Mungu ni Mungu wa maagano na watu wake, hageuki na kuacha ahadi au Agano lake na watu wake. Ndio maana mahali pengine Mungu anasema, “Mimi sitalihalifu (sitalivunja) agano langu, Sitalibadili neno lililotoka midomoni mwangu” (Zaburi 89:34). Maandiko haya yote yanaonyesha ya kuwa Mungu habadiliki.

Yesu Habadiliki

Kuhusu Yesu Biblia inasema, “Maana Mwana wa Mungu, Kristo Yesu, aliyehubiriwa katikati yenu na sisi…hakuwa Ndiyo na siyo; bali katika yeye ni Ndiyo.” (2 Wakorintho 1:19). Andiko hili linaonyesha kuwa Yesu habadiliki, na kuwa ndiyo na siyo, yeye sikuzote ni NDIYO. Andiko lingine linaloonyesha ukweli huu linasema, “Yesu Kristo ni yeye yule, jana na leo na hata milele.” (Waebrania 13:8).

Kama Alivyotenda Ndivyo Atendavyo

Kwa maandiko haya inakupasa kufahamu kuwa Mungu/Yesu habadiliki. Kama aliponya bado anaponya, kama alisamehe bado anasamehe, kama aliwapa watoto wasiokuwa na watoto bado anafanya hivyo. Watoto wako wapo kwake nawe unawapokea. Katika tatizo lako au hitaji lako ni vizuri kumfikiria Mungu vizuri. Tafuta katika maandiko aliwafanyia nini au aliwaambia nini watu waliokuwa na matatizo. Kisha ukumbuke kuwa Mungu aliyewafanyia wengine mambo mema anaweza kukufanyia na wewe. Kama vile Mungu alivyowaambia wana wa Israeli kuwa yeye ni Mungu awaponyaye (Kutoka 15:26), hajabadilika ndiye akuponyae wewe LEO. Kama vile Yesu alivyozunguka huko na huko na kuponya wagonjwa, yupo sasa karibu nawe akuponye hajabadilika. Uponyaji upo karibu na wewe. Muujiza wako upo karibu nawe maana unaye Mungu yule yule atendaye miujiza siku zote. Tarajia kuwa ameyasikia maombi yako, kama alivyowasikia watumishi wake mbalimbali katika Biblia ndivyo akusikiavyo sasa. Tegemea kupokea Muujiza kwa Mungu wa miujiza asiyebadilika, aliye dhahiri ndani yako kwa Neno lake, ingawa haonekani.

Usomapo Neno la Mungu ukumbuke ya kuwa Mungu hajabadilika, bado anatenda. Usikate tamaa bado inawezekana!. Soma vitabu vya Injili uone Yesu aliwafanyia nini wenye shida, Yote aliyofanya anakufanyia na wewe. Kwa kuwa hajabadilika na hana upendeleo.





No comments:

Post a Comment