Sunday, August 17, 2014

Agano la Kale na Jipya



Agano la Kale na Jipya
Agano la kale lilikuwa ni kivuli cha Agano Jipya lilianza wana wa Israeli walipotoka Misri kama Taifa. Walitoka baada ya Damu ya mwanakondoo wa pasaka kupakwa juu ya miimo ya milango yao. Agano hili liliisha Yesu Alipokufa msalabani kama Mwanakondoo wa Mungu na kumwaga damu yake mwenyewe kama Mwanakondoo toka juu.

Imeandikwa, “Angalia, siku zinakuja, asema BWANA, nitakapofanya agano jipya na nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda. Si kwa mfano wa agano nililoanya na baba zao, katika siku ile nilipowashika mkono, ili kuwatoa katika nchi ya Misri; ambalo agano langu hilo walilivunja, ingawa nilikuwa mume kwao asema BWANA. Bali agano hili ndilo nitakalolifanya na nyumba ya Israeli, baada ya siku zile , asema BWANA; nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika, nami nitakuwa Mungu wao nao watakuwa watu wangu. Wala hawatamfundisha kila mtu na jirani yake, wakisema mjua BWANA; kwamaana watanijua wote, tangu mtu aliye mdogo miongoni mwao hata aliye mkubwa miongoni mwao, asema BWANA; maana nitausamehe wala dhambi yao sitaikumbuka tena.” (Yeremia 31:31-33). Ni vizuri pia ukisoma maandiko yafuatayo, “Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami itatia roho mpya ndani yenu, nami nitatoa moyo wa jiwe uliopo ndani ya mwili wenu, nami nitawapa moyo wa nyama. Nami nitati aroho yangu ndani yenu, na kuwaendesha katika sheria zangu, nanyi mtazishika hukumu zangu na kuzitenda.” (Ezekieli 36:26-27).

Agano Jipya Lililo Bora
Kwa njia ya msalaba Yesu amekata Agano jipya lililobora. Sio kama lile la kwanza lililosimama kwa damu za wanyama, hili limesimama kwa damu yake mwenyewe. Sio kama lile la kwanza lililoandikwa katika gombo la chuo, na mbao za amri kumi, bali hili limeandikwa mioyoni mwa waaminio kwa njia ya roho zao kuzaliwa mara ya pili. Sio kama lile la kwanza, ambalo watu walikubaika kwa kujitahidi kushika yote yaliyoandikwa katika torati, ingawa walishindwa. Sasa tunabarikiwa kwa kuishi kwa amri ya upendo uliomiminwa na Roho Mtakatifu ndani yetu.

Upendo hutuwezasha kushika amri zote, maana mioyo yetu imefanywa upya. Sasa hivi tuna roho mpya au mioyo ya nyama iwezayo kushika amri za Mungu. Mungu alipoona watu wake wameshindwa kushika sheria kwasababu ya roho zao kufa alifungua mlango wa Agano jipya ambapo roho zitahuishwa hata kuweza kushirikiana nao na kuhusiana nao kwa kuhifadhi na kushika ayatakayo.

Sasa tunalo agano bora, Sio kama lile la kwanza ambalo watu walikubalika na Mungu kwa kuitenda sheria. Agano hili ni la Neema watu wanakubalika na Mungu na kuhesabiwa haki kwa kumwamini Yesu.

Katika Agano la kwanza Shetani alikuwa na nafasi kubwa ya kutumikisha watu katika dhambi maana asili zao zilikuwa ni roho zilizokufa. Katika Agano Jipya roho ya mtu amwaminiye Yesu huwa huru chini ya sheria ya Roho wa uzima na kufungua mlango wa kumshinda Shetani kwa uzima wa milele uliopo rohoni (Warumi 8:1-3).

Mtu amwaminiye Yesu anakuwa si chini ya sheria ya dhambi na mauti, ambayo Shetani aliitumia kutawala. Katika Agano la kwanza atendaye dhambi ilimpasa afe kwaajili ya dhambi zake. Katika Agano jipya lililobora Yesu amekufa kwaajili ya dhambi zote, wale wamwaminio wanatolewa katika adhabu ya dhambi zao, yaani hukumu.

Mungu huyu aliyetimiza ahadi alizosema katika Agano la kwanza, ambalo lilikuwa kivuli kwa kuthibitishwa kwa damu za wanyama, je ataacha kuzitimiza ahadi zake katika Agano hili lililothibitishwa kwa damu ya Mwana wake Yesu Kristo?

Agano la kwanza la Mungu na Israeli lilikuwa na makuhani wanyonge waliozuiliwa na mauti kuwa makuhani siku zote. Agano Jipya tuna Kuhani mkuu wa milele asiyeweza kufa na aliye juu. Huyu ni kuhani halisi ambaye kivuli chake kilionekana kwa kupitia makuhani wa Agano la Kale (Waebrania 7:28).

No comments:

Post a Comment