Yesu
Anitokea na Kufukuza Mashetani
Nilipofika nyumbani niliona ni vema
niombe tena Mungu, kabla sijalala.
Nilipofika usawa wa kitanda nikapiga magoti niombe, nikafanya ishara ya
msalaba. Hapo hapo nikakatisha maombi, niliona niombe kwa namna ambayo
najisikia kujieleza mimi mwenyewe kwa Mungu na si kufungwa na sala ile ya
kanisani. Niliona nimweleze Mungu hali
yangu, ilivyo nisije nikarudi tena shimoni.
Niliomba sala nyingine niliyojitungia.
Niliomba maombi mawili, nikainua mkono na kunyoosha kidole huku
naangalia macho juu nikisema, “Ee Mungu nisamehe maovu yangu yote, Nikifa Mungu
nisiende kwenye shimo nililoenda, bali niende na Yesu”
Niliposema niende na Yesu, ilitokea
ngumi ambayo sikumwona mwenye ngumi, ilikuwa hewani tu, ikanipiga
kichwani. Nikaanguka chini nikijua sasa
nimekufa, moyoni nikajisemea, hata kama
nimekufa nitaenda na Yesu. Sikufa ila
nilitetemeka hata asubuhi, kulipokucha nilijua mchana wakati wowote naweza
kufa.
Asubuhi nikamwambia mke wangu twende
shambani. Nilikuwa na maana ya kwenda
shambani kuliangalia mara ya mwisho. Tuliporudi
mke wangu alitengeneza chakula, tulikula huku nikiwa na huzuni nikijua
ninamwacha na motto mmoja tuliyekuwa naye.
Baada ya hapo mama akatoka nje, ilikuwa ni kwenye saa tisa ya mchana. Niliingia chumbani nikakaa kitandani.
Nikawaza mbona nimeteseka miaka yote! Acha nife tu, acha nife tu. Mbona hata Karume amekufa, kipindi hicho
Karume raisi wa Zanzibari, alikuwa amekufa muda si mrefu. Maneno haya aliyokuwa akisema mtumishi afe tu afe tu, hakuwa yeye,
mashetani yalikuwa yakisema katika nafsi yake kwa sura yake yeye. Shetani hutumia akili zetu kusema nasi kama nafsi zetu wenyewe. Ukiweza
usome kitabu cha Mitego ya Shetani nilichokiandika upate ufafanuzi zaiji
jinsi atendavyo.
Wakati naendelea kuwaza hivyo upepo
ulivuma na nikaona kipeperushi cha injili (traks) kimeletwa na upepo kikatua
chumbani, nikasikia sauti moyoni ikisema chukua hiyo, chukua hiyo uisome. Sauti hii ni kama
ile iliyoniambia, “Tazama juu” nilipokuwa shimoni. Nyumba yetu ilikuwa ya kienyeji ina dirisha
dogo, nikatoka nje kuisoma nikasimama mlangoni niisome.
Roho
ya Mauti
Nikaianza kuisoma msitari wa kwanza
uliandikwa, “Yesu Kristo ni Mwokozi”.
Niliposoma tu, nikapigwa ngumi tena kama
usiku! Nikaingia chumbani huku
ninatetemeka. Nilipofika usawa wa kitanda nikaanguka kitandani. Nilipopandisha miguu kitandani nikaona
kitu. Niliona lidude kama
binadamu, lakini si binadamu. Lilikuwa kubwa na lenye nguvu mtu asiweze
kushindana nalo. Kwa kulitazama liliweza
hata kushinda watu elfu kwa mara moja. Likanishika kinywa na pua nishindwe
kupumua. Nikasema wakati linaziba pua na mdomo, “Ikiwa Shetani anauwa nitakufa,
lakini shimoni siendi naenda na Yesu”
Nilipotamka naenda na Yesu likaniachia na kukimbia kwa hofu!
Likarudi tena mara ya pili na kuniziba
pua na mdomo, nikasema tena kwa ujasiri na nguvu zaidi kama
nilivyosema kwanza, likakimbia tena kwa hofu.
Nikagundua kwamba nikisema naenda na Yesu linaogopa sana na kukimbia. Nikajipanga kama likija mara ya tatu nitasema
kwa ujasiri na nguvu zaidi. Lilipokuja
mara ya tatu nikasema kwa nguvu na ujasiri zaidi, “Naenda na Yesu” Lilikimbia
na kupotea kama ndege arukaye kwa kasi.
Yesu
Atokea
Niliamka kitandani nione lile jitu
limekimbilia wapi, nilipoamka nilikuta kumbe kuna mtu amesimama pembeni ya
kitanda. Alikuwa na vazi jeupe linalong’aa
na kutingishika tingishika. Katikati ya
vazi hilo kulikuwa na mkanda uliong’aa na
miguuni alikuwa na viatu vizuri ambavyo havifanani na viatu vya duniani,
vilikuwa ni kama viatu vya kamba za
ngozi. Nywele zake zilikuwa nyeupe,
lakini weupe wa aina yake tofauti na weupe wa vazi alilovaa; Zilianguka mgongoni mwake. Weupe wake haukufanana na weupe walionao
binadamu wa kawaida. Huwezi kusema ni mzungu, muhindi mwafrika au mchina, alikuwa
“neutral” Macho yake yalikuwa makali yanayong’aa.
Tukatazamana macho kwa macho
nikamwangalia kwa makini. Mara!
akanyosha mkono wake wa kulia na kusema, “Ninyi
mashetani mnataka mumfanye nini mtu huyu.” Nikashangaa likatoka lijitu
lenye umbo la mwanaume lilikuwa refu na jeusi tii! Wakati naendelea kushangaa likatoka lingine
lilikuwa jeusi fupi na nene! Nikajiambia
mwenyewe kwa mshangao nilikuwa na watu ndani yangu! Walikaaje kaaje? Huyu mfupi
mnene alikuwa akitembea na kuangalia nyumba huku anaondoka yule wa kwanza
alikimbia haraka zaidi. Baadaye
nikaaacha kuyaangalia yale mashetani na kugeuka nitoe shukrani kwa Yesu,
nikakuta ameshatoweka! Nilijisikia mwepesi sana, kichomi kikaisha na ugonjwa wa muda mrefu
uliokuwa ukinisumbua ukaisha, Hofu ya kufa tokea hapo ikaisha.
Katika
ushuhuda uliopita tunajifunza yafuatayo kwa neno la Mungu. Kwanza
ni Yesu anaona kila kitu ndani yetu (Waebrania 4:12-13). Alimkazia macho mtumishi wake kumbe ameona
mashetani ndani yake. Kitu cha pili tunajifunza Yesu anayo mamlaka juu ya
mashetani, alisema tu mnataka kumfanya nini huyu mtu na yakatoka. Leo
tunapotumia jina lake anatenda kama yupo hapo hapo, jina lake
mbele za mashetani ni yeye mwenyewe
kwa kuwa lilipo jina lake
na yeye yupo(Marko 9:37,
Mathayo 18:20). Kama aliyauliza tu yakatoka na sisi tukiyaamuru kwa jina lake yatatoka
(Marko 16:17). Kitu kingine tunachoweza kukiona katika ushuhuda huu ni kwamba
pepo wanazo ngazi na vyeo. Hukaribishana ndani ya mtu. Inawezekana kabisa yule aliyemtoka wa mwisho
aliyekuwa mfupi ndiye aliyekuwa mkubwa, maana aliondoka huku akiangalia angalia
alipotoka. Jambo lingine tunalojifunza ni kwamba si kila ugonjwa ni ugonjwa tu,
mwingine ni mashetani yanakuwa yapo ndani ya mtu na yanasababisha kuumwa.
Nikaitafuta ile traks, niisome nione kama nitapigwa tena ngumi. Nilisoma na kuimaliza hakuna kilichotokea tokea wakati huo, ugonjwa
ulionitesa miaka sita uliisha nikafunguliwa kabisa. Siku hiyo aliponitokea Bwana nilisema,
kuanzia sasa niwe mpole na mzuri kama
aliyeniponya. Nikajiambia nitakuwa naenda kanisani na kuwa mtakatifu kama yeye alivyo.
Muda ulipita siku moja haya mashetani
yalirudi tena. Yalianza kunishawishi niyakubali tukae nayo na yatanifanya niwe
tajiri nisipate shida tena. Walinishawishi niachane na mambo ya kuokoka, Yalisema
nimewahuzunisha mno ndugu zangu. Wakati
huu majitu haya yalikuwa yamevaa nguo kama za
kijeshi. Nikawajibu kwa ujasiri “hakuna
kurudi nyuma” Waliondoka hawakurudi tena.
Katika
ushuhuda uliopita tunajifunza kwamba Shetani hutumia heshima, Mali na watu wanavyotuona ili
atupate. Hata Yesu alimwambia
akimsujudia atampa yote yaliyopo duniani (Mathayo 4:9). Lakini Yesu ametufundisha akisema, uzima wa
mtu haupo katika wingi wa vitu alivyo navyo (Luka 12:15). Kuwa na mali na fedha hakutuokoi, Yesu ndiye
utajiri, tukae kwake yeye aliye ufalme wa Mungu atatuzidishia yote (Mathayo
6:33). Utajiri ulio nao mkubwa ni nafsi
yako kutopotea kwa njia ya Yesu Kristo. Nafsi yako ina thamani kuliko vyote
unavyoviona duniani! Kwa hiyo Shetani asikudanganye ukaiuza nafsi yako kwa
kumwasi Mungu kwa vitu vyenye thamani ndogo kuliko wewe navyo ni mali
na fedha. Hivi Bwana mwenyewe atatupa, ila hatutajiuza na kumfuata Shetani ili
tuvipate..
No comments:
Post a Comment