Saturday, June 21, 2014

Msingi wa Nguvu ni Tabia



Kutunza Huduma

“Mwambieni Arkipo, iangalie sana huduma ile uliyopewa katika Bwana, ili uitimize”
(Wakolosai 4:17)
1. Unachofanya na Tabia
Lolote utendalo linadumu kwa njia ya tabia uliyo nayo.  Ikiwa wewe ni mwanafunzi na una akili, tabia yako inaweza kufuta kila kitu ukaonekana ni mpumbavu.  Ikiwa wewe ni mfanyakazi na una ujuzi mkubwa tabia yako yaweza kukuharibia sifa zako zote za ujuzi. Ikiwa wewe umeokoka au ni mtumishi wa Mungu tabia yako ndiyo inayoshika huduma kama msingi, sio vipawa na karama.  Paulo alimwambia mtoto wake wa kiroho Arkipo aiangalie sana huduma aliyopewa katika Bwana. Naamini njia moja wapo ambayo angeweza kuiangalia ni kwa kujijengea tabia nzuri.
A. Nyumba na Msingi
Kama vile nyumba isivyoweza kusimama bila msingi, kazi yako au huduma haiwezi kusimama bila tabia.
B.Mti na Mizizi
Kama vile mti hauna maana bila mizizi, huduma yako na ujuzi wako wote hauna maana kama hujajenga tabia njema inayoambatana nao.
2. Jenga Tabia Kabla ya Huduma
Kuna watu wakubwa na wenye nguvu na vipawa lakini havikuwasaidia, hawakudumu kuwepo kwasabadu ya tabia; Mfano Sauli, Samson, Yuda Iskariote, nk ( Waamuzi 13:24-25, 14:1-19, 1Samwel 14:47-48, 1Samwel 15:1-24).  Sauli alikuwa mfalme mwenye nguvu, tabia yake ilimwondoa katika ufalme, kwa kukaidi kufanya alichotaka Mungu. Angeweza kuendelea kuwa mfalme ikiwa tabia yake ingeendelea kuwa njema. Samson alikuwa na nguvu za kupigana kwa uwezo wa Mungu, tabia yake ilimponza akatobolewa macho na nguvu zake zikaisha. Angeweza kuendelea kuwa na nguvu ikiwa tabia yake ingeendelea kuwa njema.
3.Jinsi ya kujenga Tabia njema
1. Fahamu udhaifu wako na uuseme wazi mbele za Mungu, usijifiche wala kujitetea (Waebrania 12:1).
2.Azimia kusema ukweli wakati wote, tabia kubwa ya Shetani ni uongo (Yohana 8:44).
3.Tambua hakuna siri, chochote ufanyacho, mahali popote unaonekana (Waebrania 4:13).
4.Watakie watu wote mema tokea moyoni na si kinywani tu (Mathayo 7:12).
5.Uwe tayari kukosolewa na kurekebishwa(Waebrania 12:7-13).
6.Usiangalie kwa macho yako picha za uchafu, na kusikiliza vitu vibaya, tabia hujengwa na kitu unachotazama mara kwa mara na kusikiliza (Zaburi 101:3).
7.Soma Neno la Mungu na kulisikiliza wakati wote (Mithali 4:20-21).
8.Uwe na taadhari na rafiki anayekushusha moyo na kusema vitu vibaya vya watu kila wakati(1Wakorintho 15:33).
9.Ufikirie mwili wa mtu wa jinsia tofauti nawe kuwa ni nyumba ya Mungu inayoheshimika (1Wakorintho 3:16)
10. Usidhibitiwe na misukumo ya ndani kama hamu ya kula, kutaka heshima, kutaka kujamiiana, hii ipo ila iko chini yako, isikuweze (1Wakorintho 6:12, 10:23).
11.Uwe na nidhamu na tayari kuumia kwaajili ya malengo uliyojiwekea (1 Wakorintho 9:25-27).
12.Tambua huwezi na hujui kila kitu, unamuhitaji mtu mwingine (1Wakorintho 12:27)
Ufanyapo Haya na Mengine atakayokuonyesha Roho Mtakatifu, utajenga tabia njema, kisha utadumu kuwepo katika yale uyafanyayo, hutaishia njiani, kama ni katika huduma, biashara au kazi.

No comments:

Post a Comment