Thursday, June 19, 2014

Kutana na Watu Ukutane na Yesu



Dexomai

Awapokeaye ninyi, anipokea mimi, naye anipokeaye mimi, ampokea yeye aliyenituma  (Mathayo 10:40)

Katika  andiko hili neno “awapokeaye”  kwa Kiyunani ni “dexomai”.

Maana ya neno hili ni:awakubaliye, awakumbatiaye, awathibitishaye, awapaye sikio lake au awasikilizaye.

Kwa msingi Yesu alikuwa anaonyesha mtu amkubaliye mtumishi wa Mungu, na kumthibitisha, pamoja na kumwonyesha upendo, na  amsikilizaye.  Hufanya hivyo kwa Yesu, na afanyaye hayo kwa Yesu hufanya kwa  Mungu Baba.

Wazo Kuu
Tufanyapo haya kwa watumishi tunachochea uwepo na kibali cha Mungu katika maisha yetu. Mtumishi si muhubiri tu, bali kila aliyempa Yesu maisha anao wito. Kwa kufanya haya hatimaye tutaishi na Mungu wakati wote. Usisubiri kumwona Mungu kwa macho! Heshimu, mpende, msamehe, mjali, mwombee, usitegemee mambo mabaya tu, na kufikiria mambo mabaya kuhusu watu wa Mungu. Mungu ametuandika majina katika kitabu cha uzima, baada ya kuwa ndani ya Yesu, ingawa ni watu tuliopo duniani. Hii inaonyesha anategemea mambo mazuri kwetu. Mtangulize mtu yeyote aliyempa Yesu maisha yake, muone anafaa, usiangalie na kufikiria makosa na dhambi zake, Fikiria kifo cha Yesu kwaajili yake. Mwonye kwa upendo, jiombee kabla ya kumwonya na kumwombea, uwe mtu mwema kwa watu wote, hasa wale waaminio, uwe mpatanishi na si mchonganishi. Ufanyapo hayo utaishi na Yesu hapa duniani, Moyo wako utakuwa mweupe! Pia ufanyapo hayo utafanyiwa hayo. Kipimo cha kutaka ufanyiwe jambo ni kuanza kuwafanyia wengine ( Mathayo 7:12).

Mtendee Yesu mema kwa watu ulionao, kipimo cha kumjua Mungu na kumwona ni jinsi unavyowaona na kuwachukulia watu wengine, wachukulie kama ni Yesu, ukijua anawapenda wote.

SOMA TENA, OMBA  NA KUTAMKA MANENO HAYA KABLA YA KUANZA KAZI ASUBUHI, PIA KABLA YA KULALA TAFAKARI, AU SHIRIKISHANENI KATIKA KIKUNDI NA IBADA YA NYUMBANI.

No comments:

Post a Comment