Saturday, April 20, 2019

MEZA YA BWANA::SEHEMU B: I. YALIYOMO NDANI YAKE

Meza ya Bwana ina mambo kadhaa ndani yake:

AGANO JIPYA

Agano la Kale lilianzwa kwa damu ya kondoo wa pasaka kumwagika na torati kutolewa katika mlima Sinai. Alama yake kwa Waisraeli ilikuwa ni tohara.

Agano jipya limeanza kwa damu ya Yesu ilipomwagika, na Roho Mtakatifu kuja kwa wanadamu. Alama yake ni kuzaliwa mara ya pili, roho zetu kufanywa upya kwa njia ya Imani zetu kwa Yesu, “Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa Mungu kwa njia ya Imani katika Kristo Yesu.” (Wagalatia 3:26).

Damu ya Yesu ni damu ya Agano Jipya imwagikayo kwa ajili ya ondoleo la dhambi. Kwahiyo tunaposhiriki mwili na damu ya Yesu twalionyesha Agano Jipya. “kwa maana hii ndiyo yangu ya Agano, imwagikayo kwaajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi”(Mathayo 26:28). Tunaposhiriki meza ya Bwana twalionyesha Agano la Ibrahimu na pia Baraka ya Ibrahimu. Hii ni kwa Mataifa yote kwa njia ya Yesu Kristo. Baraka hii inaonekana sehemu mojawapo katika Agano jipya, inaonekana kuwa ni kuepusha dhambi au kumgeuza kwa njia ya Yesu, “Ninyi mmekuwa watoto wa manabii na wa maagano yale, ambayo Mungu aliagana na baba zenu, akimwambia Ibrahim, katika uzao wako kabila zote za ulimwengu zitabarikiwa. Mungu, akiisha kumfufua mtumishi wake Yesu, alimtumakwenu ninyi kwanza ili kuwabarikia kwa kumwepusha kila mmoja wenu na maovu yake” (Matendo 3:25-26). Baraka ya Ibrahimu kwa kupitia Uzao Yesu Kristo imetokea kwa njia ya Yesu kufufuka, kwa Yesu kufufuka tumepata ondoleo la dhambi na tumegeuzwa toka katika dhambi. Yote aliyoyapata Yesu kwa kufufuka ni Baraka aliyoahidiwa Ibrahim, inawafikia Mataifa yote kwa Imani katika huyu Yesu ndani ya neno la injili. Meza ya Bwana imeyashika yote haya, katika Agano Jipya!

Tafrisi nyingine ya neno hili ondoleo la dhambi ni Baraka ya Ibrahim, maandiko yanasema Mungu akiisha kumfufua yesu katika watu alimtuma ili kutubarikia Baraka ya Ibrahimu kwa kumwepusha kila moja wetu na dhambi zake, kitu ambacho damu ya Yesu iondoayo dhambi zote kwa kila amwaminie. Damu hii pia ni ya agano jipya, utimilifu wa Baraka ya Ibrahimu upo Agano Jipya katika mzao Yesu Kristo kwa mwili na damu yake .

KUTANGAZA MAUTI

Mauti ya Yesu msalabani imelipia maisha yetu yote. Imelipia maisha yetu yaliyopita, ya sasa na yajayo. Imemuharibu Shetani kabisa. Hukumu ya dhambi haipo juu yetu tena, Yesu alipouwawa alilipa hukumu yetu ya kifo kwaajili ya dhambi zetu. Tulitakiwa na sheria tufe kwaajili ya dhambi zetu. Yesu akafanyika dhambi zetu akafa badala yetu.

Kutangaza mauti ya Yesu ni kutangaza ushindi wake na ukombozi wake mpaka ajapo. Kuhusu kutangaza mauti yake imeandikwa, “Maana kila mwulapo mkate huu na kukinywea kikombe hiki, mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo” (1Wakorintho 11:26). Neno kutangaza hapa linamaana ya kuonyesha mauti ya Yesu hata ajapo. Mauti ya Yesu msalabani imetulipia kila kitu, mbele za Mungu, sheria na Shetani. Kuitangaza kila mara ni ujenzi na uthabiti mkubwa wa Imani zetu. Kutotangaza mara kwa mara mauti ya Yesu ni kutojali alichotufanyia. Kutangaza huku kunaambatana na shukrani za mara kwa mara kupitia meza ya Bwana tunayoishiriki mara kwa mara. Andiko hili liliposema kila “mwulapo mkate” kwa tafsiri ya Kiingezera ina maana mara kwa mara muulapo mkate, mwaitangaza mauti ya Bwana. 

Kutangaza mauti ya Kristo ni kutangaza mwisho wa utawala wa Shetani, ni kutangaza mwisho wa utawala wa sheria, ni kufunga mwisho wa utawala wa mwili wa dhambi au tamaa, ni kutangaza kufufuka kwa Yesu katika wafu. Tangazo hili lipo tunaposhiriki meza ya Bwana.

MARA KWA MARA

Kama tulivyoona, Kila mwaka wana wa Israeli walishiriki sikukuu ya pasaka. Hii ilikuwa sura ya ukumbusho wa ukombozi wao. Kwa upande mwingine mara kwa mara walikula mana, ndani ya kila masaa ishirini na nne, picha zote hizi mbili zinabeba meza ya Bwana.

Katika Matendo 20:7 imeandikwa, “Hata siku ya kwanza ya juma, tulipokuwa tumekutana ili kumega mkate, Paulo akawahutubu…”. Siku ya kwanza ya juma ilikuwa ni Jumapili. Inaonekana Kanisa lilikuwa na utaratibu wa kushiriki meza ya Bwana kila siku ya kwanza ya juma. Hapa anasema walikusanyika siku ya kwanza ya juma ili kuumega mkate. Sababu moja wapo ya wao kwenda kukusanyika ilikuwa ni kumega mkate. Kwa maana hii inaonyesha walishiriki mara kwa mara.

Imeandikwa tena, “Wakawa wakidumu katika fundisho la mitume, na katika ushirika, na katika kuumega mkate na katika kusali” (Matendo 2:42). Angalia mambo ambayo kanisa hili lilidumu au lilifanya wakati wote: Fundisho, ushirika, meza ya Bwana, Maombi. Kwa kuongezea angalia na andiko hili, “Na siku zote kwa moyo mmoja walidumu ndani ya hekalu wakimega mkate nyumba kwa nyumba na kushiriki chakula chao kwa furaha na kwa moyo mweupe.” (Matendo 2:46). Angalia na hapa neno hili “sikuzote”, linataka kufanana na lililopita “wakidumu”. Hii inaonyesha walishiriki meza ya Bwana mara kwa mara.

Ni wapi ambapo walishiriki? Walishiriki katika masinagogi na nyumba kwa nyumba. Meza ya Bwana inaweza shirikishwa kanisani au hata nyumbani. Hapa sitoi mwongozo au sheria bali mlango wa mtu kuweza kuitumia mara kwa mara. Agano la Kale sikukuu ya Pasaka ilianzwa kufanyika nyumbani. Baba, yaani kiongozi wa familia ndiye aliyehusika na maandalizi na usimamizi wa sikukuu ya Pasaka na mikate isiyotiwa chachu. Sio kitu kibaya ikiwa nyumbani wote mmeamini na mnaishi katika Bwana kushiriki pamoja mwili na damu ya Yesu.

Somo hili linaendelea, jiunge nasi kila wiki na kila siku kwa masomo mengine mbali mbali katika blog hii. karibu kwa Maswali, Maoni na Wajulishe Wengine, Tujifunze na kukua pamoja. 
Barikiwa.

No comments:

Post a Comment