Muda si mrefu kutoka sasa, nitatoa kitabu hiki cha Imani na Kuhesabiwa haki. Usikose kukisoma. Nimeonyesha utangulizi wake na sura ya kwanza hapa.
UTANGULIZI
Leo
tarehe 02/07/2015, nilipokuwa naomba kwa kunena kwa lugha asubuhi, niliona
maandishi moyoni yaliyokuja ghafla “Imani
na kuhesabiwa haki”. Hapo hapo nikajua hilo ni somo ambalo lapaswa liwe
kitabu. Wakati naendelea kunena kwa lugha likaja somo lingine liitwalo “Dawa ya Imani”. Haya ni masomo mawili yaliyokuja wakati mmoja! Ingawa kwa
sasa tutajifunza somo hili la imani na kuhesabiwa haki.
Maandiko
yanonyesha tumehesabiwa haki kwa Imani ya Yesu Kristo. Msingi wa haki yetu
mbele za Mungu ni Imani katika Yesu Kristo. Hii ndiyo tofauti kubwa ya Agano la
Kale na Agano Jipya. Agano la Kale lilikuja kwa ajili ya Wayahudi na lilikua la
SHERIA. Mtu akitenda SHERIA, basi angehesabiwa haki. Agano Jipya ni kwa ajili
ya dunia nzima na sio kwa Wayahudi tu, katika Agano hili mtu anahesabiwa haki
kwa IMANI. Maandiko yanasema, “(28)Basi, twaona ya kuwa mwanadamu huhesabiwa haki kwa
Imani pasipo matendo ya sheria. (29)Au je! Mungu ni Mungu wa Wayahudi tu? Siye Mungu wa
Mataifa pia? Naam, ni Mungu wa Mataifa pia; (30)kama kwa kweli Mungu ni mmoja,
atakayewahesabia haki wale waliotahiriwa katika Imani, nao wale wasiotahiriwa
atawahesabia haki kwa njia ya Imani iyo hiyo.”(Warumi
3:28-30). Katika Yesu, baada ya kumpa
maisha yetu, msingi wetu wa ushirika na yeye wenye nguvu kwa mtu aliyeokoka ni
kufahamu kuhesabiwa haki kwa Imani maana yake nini.
Usiache
kusoma na kuelewa somo hili la kuhesabiwa haiki kwa Imani. Ufahamu kuhusu
kuhesabiwa haki ni kama nguzo ya katikati ishikayo nyumba yote. Wokovu wako
wote unaweza kushikwa na kutotikisika kwa ufahamu wa kuhesabiwa haki kwa Imani.
Katika
Sheria iliwapasa binadamu (Wayahudi) kufanya kitu kwa kuitii Sheria ili
wahesabiwe haki. Katika Agano Jipya, Yesu amefanywa kwetu jambo fulani ili sisi
tuhesabiwe haki tunapomwamini, sasa hatufanyi sisi amefanyika Yesu, “Bali kwa yeye ninyi mmepata kuwa katika
Kristo Yesu, aliyefanywa kwetu hekima itokayo kwa Mungu, na haki, na utakatifu,
na ukombozi” (1Wakorintho 1:30).
I
MAANA YA KUHESABIWA HAKI
Maandiko
yanasema, “kwa sababu wote wamefanya
dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu; (Warumi 3:23). Binadamu wote
wametenda dhambi mbele za Sheria ya Mungu. Wanadamu ni watenda dhambi kwa
sababu kuu moja: Ni watenda dhambi kwa sababu wamezaliwa katika dhambi. Dhambi
ipi?Ni dhambi ya Adamu. Adamu alipokosea watu wote waliokuwa ndani yake katika
mbegu (wewe na mimi), tulikosea. Wote tulitenda dhambi, Adamu alipotenda
dhambi. Maandiko yanasema, “Kwa sababu
kama kwa kuasi kwake mtu mmoja watu wengi waliingizwa katika hali ya wenye
dhambi, kadhalika kwa kutii kwake mmoja watu wengi wameingizwa katika hali ya
wenye haki.” (Warumi 5:19). Mtu ni mtenda dhambi siyo kwa sababu anatenda
dhambi tu, la! Ni mtenda dhambi kwa sababu amezaliwa na dhambi ametoka kwa
Adamu mwenye dhambi.
Dhambi
watu wanazotenda kama kuiba, kuua, kuzini, kusema uongo nk, Siyo msingi unaowafanya
wawe wenye dhambi, ni wenye dhambi kwa kuwa wameazaliwa katika dhambi,
wamezaliwa toka kwa Adamu mwenye dhambi. Hizo dhambi wanazotenda ni matunda tu
yanayoonekana, mzizi wake hauonekani, huu ndiyo tatizo, unaitwa dhambi ya Adamu
ndani yao. Adamu alipotenda dhambi
wote tulikuwa watenda dhambi na kuzaa matunda ya dhambi.
Dhambi ya Adamu
Tunaposema
dhambi ya Adamu tunamaanisha nini? Kitabu cha Mwanzo 2:16 – 17 na Mwanzo 3:6
kinaonyesha Adamu aliasi alichosema Mungu hii ilikuwa ni dhambi iliyopandwa
ndani yake na kuwafikia watu wote. Watu wote waliasi alichosema Mungu, waliasi
kwa kuwa wote walikuwa ndani ya Adamu. .
Adamu
na Eva, Waliasi kwa ushawishi wa nyoka (Mwanzo 3:1) au Shetani (Ufunuo 12:9). Wangeweza
kupingana na uasi huo au ushawishi huo kwa kutumia Neno la Mungu alilosema nao, “BWANA Mungu akamwagiza huyo mtu,
akisema, matunda ya kila mti wa bustani waweza kula, walakini matunda ya mti wa
ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo
utakufa hakika.” (Mwanzo 2:16-17). Lakini hawakutumia maneno haya kumpinga Shetani,
bali walikubali kudanganywa. Hii inatufundisha nini? Dhambi huwezi kuipinga
bila Neno la Mungu. Ushawishi wa kishetani huwezi kushindana nao bila Neno.
Mungu aliposema nao na kuwaambia matunda ya kila mti waweza kula ila mti wa
ujuzi wa mema na mabaya wasile, aliwapa Neno ambalo wangeweza kulitumia kupinga
ushawishi wa kishetani na kupinga dhambi. Pengine ndiyo maana Daudi alisema
ameliweka Neno moyoni mwake asije kumtenda dhambi (Zaburi 119:11).
Jinsi
Adamu na Eva walivyoshindwa kutumia Neno alilowapa Mungu ili kupinga ushawishi
wa Shetani, ndivyo Yesu alivyoshinda kwa kutumia Neno na kupinga ushawishi wa
nyoka /Shetani (M
athayo
4:1-11). Kwa hiyo twaweza kusema dhambi ya Adamu ni uasi wa Neno la Mungu
alioufanya Adamu. Huu ulipelekea kumuua kiroho na kuingiza kifo duniani. Dhambi
hii ipo kwa wanadamu wote, imeingia kwao kwa mtu aitwaye Adamu. Inaondoka kwa ‘mtu’
aitwaye Yesu Kristo (Adamu wa pili).
Kuhesabiwa Haki
Kuhesabiwa
haki ni neno la kisheria, ambalo linaonyesha hali ya kuonekana mbele ya sheria
kwamba mtu hana hatia. Kuhesabiwa haki ni kumwachilia mtu toka katika hatia.
Kwa mfano mtu amekosea anatakiwa auawe kwa kuwa ameua. Halafu akatamkwa kwamba
hana hatia hatakiwi kufa tena! Kitendo cha namna hii kikitokea, basi
amehesabiwa haki. Neno la Kiyunani dakaioo,
limebeba maana hizi ambalo tafsiri yake ni: kufutia
na kuonyesha hali ya kutokuwa na hatia, kuweka huru mbali na hatia, kufanya mtu
asiwe amekosea wala asiwe na hatia.
Katika
Sheria ya Mungu mtu hawezi kuachiliwa hivi na kutamkwa hivi bure! Lazima tamshi
hilo lilipiwe. Maandiko yanasema mshahara wa dhambi ni mauti (Warumi 6:23).
Haiwezekani mtu akatamkwa hana hatia bila dhambi zake kulipiwa na mauti. Ikiwa
Mungu angetutamka kuwa hatuna hatia wakati tumefanya dhambi ya Adamu istahiliyo
kufa, basi asingekuwa mwenye haki katika sheria yake.
Hivyo
ilikuwa ni lazima, ili Mungu aweze kutuhesabia haki na yeye aendelee kuwa
Mwenye haki, dhambi zetu zilipiwe kwanza kwa kifo. Kifo hiki alikufa Yesu
asiyekuwa na dhambi. Njia ya zamani ya kuingia mbinguni ilikuwa matendo ya Sheria,
yaani kuitenda Sheria yote ya Musa, hii ilishindikana. Yesu ndiye njia mpya ya
kuingia, njia hii imewezekana, “Yesu
akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia
ya mimi.” (Yohana 14:6), Pia soma Waebrania 10:19-20.
Kuna
tajiri mmoja katika maandiko anaonekana alizishika amri na kuzitegemea ili
amwone Mungu hii ilishindikana. Yesu akaonyesha ilimpasa auze vyote, asitegemee
chochote kisha amfuate Yesu. Tajiri alishindwa, hapo hapo akaonekana alipenda
mali kuliko Mungu. Akavunja amri ya kwanza wakati alisema amezishika zote!
(Soma Mathayo 19:26). Hakutakiwa kutegema chochote bali Yesu tu, ili amwone
Mungu. Yote aliyoyafanya kwa kushika Sheria hayakumsaidia. Kuhesabiwa haki kwa
Imani maana yake ni Yesu tu anatosha ili
Mungu akukubali na usiwe na hatia mbele zake, na siyo kitu kingine chochote. Ni
kwa Imani katika Yesu tu!
Haki ni Kipawa
Kuhesabiwa
haki ni kuokoka. Fananisha maandiko haya mawili utagundua kwamba kuhesabiwa
haki ni kuokoka. Matendo 16:31 na Matendo 13:38. Katika andiko la kwanza
(Matendo 16:31), imeandikwa mwamimini
Yesu Kristo nawe utaokoka na nyumba yako. Kumwamini Yesu kunaleta
kuokolewa. Andiko la pili (Matendo 13:38-39), linasema mtu akimwamini Yesu atahesabiwa haki. Kwa hiyo kumwamini Yesu
huleta wokovu au kwa lugha nyingine, wokovu huu unaitwa kuhesabiwa haki. Kwa kuunganisha maandiko haya na kuyatafsiri
tunajifunza kwamba kuokoka ni kuhesabiwa
haki kwa njia ya kumwamini Yesu. Kuokoka ni zawadi ni kipawa, kuhesabiwa haki
pia ni zawadi ni kipawa, Warumi 5:17, inaita haki ni kipawa. Haki tunayopewa
katika Kristo tunapewa kama zawadi iliyotolewa kwa neema ya Kristo kufanyika
dhambi, ili sisi tuwe haki ya Mungu katika yeye. Sisi hatujahesabiwa haki tu,
tumekuwa haki ya Mungu, baada ya Kristo kuwa dhambi zetu.
No comments:
Post a Comment