Saturday, July 4, 2015

Imani Husema



Ukiri wa Imani

Katika agano jipya kuna mambo Yesu alikuja kuyafanya kwaajili yetu, ambayo tukiykiri kwa imani tutakuwa tunaachilia nyugu ya Agano. Kila nikiamka asubuhi au kabla ya kulala huyakiri haya naamini nitafanya hivyo maisha yote. Karibu na wewe kukiri haya ili tuliishi Agano kwa imani. Mambo haya Roho Mtakatifu alinifundisha tarehe 19.9.2010 nilipokuwa na hudumu maeneo ya Sagara Singida. Mwili na damu ya Yesu ndio chanzo cha Agano jipya. Kabla hujashiriki meza ya Bwana unaweza kuyakiri mambo haya na yatathibitika kwako kama Agano. Utakuwa ukifanya ukumbusho wa kazi ya Yesu aliyoifanya msalabani kwa mwili na damu kwaajili yako.

Sema Yesu Alimfanya Nini Shetani Kwaajili Yako
  1. Alimharibu kwa mwili wake kwaajili yako (Waebrania 2:14). Sema hivyo.
  2. Aliziharibu kazi zake zote kwaajili yako (1Yohana 3:8). Sema kama neno lisemavyo.
  3. Alimfanya si Kitu akamnyanganya silaha kwaajili yako (Wakolosai 2:15). Patana na andiko hili na kulisema.
  4. Yesu alituokoa toka katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake. Sema Yesu ameniokoa toka nguvu za giza nipo ndani ya ufalme mwingine, ufalme wa Mungu (Wakolosai 1:13-14).
  5. Alimfadhaisha Shetani hadharani (Wakolosai 2:15). Sema haya, aliyafanya kwaajili yako. Unaweza kuongezea maandiko mengine.

Sema Yesu Alifanya nini mbele za Mungu kwaajili yako
  1. Aliingia mbele za Mungu kwaajili yako, sema unaweza kuingia hapo kwa ujasiri (Waebrania 9:24). Sema kama neno lisemavyo.
  2. Aliharibu mashitaka ya Torati iliyokuwa inanishitaki mbele ya haki ya Mungu. Aliharibu kwa njia ya kuyasulubisha mashitaka yake kwa yeye kufanyika dhambi na kusulubiwa (Wakolosai 2:14). Tamka kwamba imetokea kwako, torati haina nguvu kwako.
  3. Sema Yesu alifanya amani mbele za Mungu kwa damu ya msalaba wake. Ninaweza kumkaribia Baba bila woga kwa damu ya Yesu (Wakolosai 1:20).
Sema Wewe ni nani katika Yesu
  1. Sema “Mimi ni mjumbe ni balozi wa Mungu”. Sema “Nipo duniani kusema kwaajili ya mbinguni” (2Wakorintho 5:20).
  2. Sema “Nimezaliwa kwa mbegu ya mbiguni neno la Mungu ninafanana na Neno lake” (1Petro 1:23).
  3. Sema “Nimenunuliwa kwa damu ya thamani, hiyo inaonyesha uthamani wangu, sijanunuliwa kwa fedha bali kwa maisha ya Mungu, yaani damu yake” (1Petro 1:18-19).
  4. Sema “Wenyeji wangu ni mbinguni sio duniani. Ninazo hali za mbinguni si za duniani” (1Petro 2:9). Unaweza kuongezea maandiko.

Sema Una kitu gani ndani ya Yesu
  1. Sema ninayo Amri ya kukanyaga nyoka na nge na nguvu zote za giza (Luka 10:19).
  2. Ninalo tumaini la uzima wa milele kwa njia ya Yesu kufufuka katika wafu (1Petro 1:3).
  3. Sema ninao uzima wa milele, nguvu ambayo inamfanya Mungu awe Mungu (Yohana 3:16).
  4. Sema Bwana ni mchungaji wako hautapungukiwa unayo unayohitaji (Zaburi 23:1-2).
  5. Unaye Mungu aliye upande wako hakuna aliye juu yako, sema hivyo (Warumi 8:31).
  6. Sema aliye ndani yako ni mkuu kuliko aliye katika ulimwengu. Roho wa Mungu, Yesu Kristo, Mungu Baba ndani yangu ni mkuu. Mkuu kuliko uchawi, pepo na uharibifu wote (1Yohana 4:4).
Mfumo wa ukiri katika maisha yako unaweza kuuanza kupitia mambo haya manne. Ukianza kukiri Mungu atazidi kukupa ufunuo na imani yako itaongezeka. Ongezea maandiko hayatoshi haya niliyoyataja. Kiri kila unapoamka au kabla ya kulala. Unaposoma Biblia hasa Nyaraka za Mitume ongeza maandiko. Baada ya muda kupita utaongeza imani yako na kushinda kwa ukiri wa imani.
     Kuhani wa Maungamo
Yesu ni kichwa cha Kanisa ni kuhani wetu    mkuu mbele za Mungu. Amekwenda mbinguni kwaajili yetu, yupo mkono wa kuume wa Mungu kwaajili yetu.  Je, tunaunganishwa naye kwa jinsi gani? Ni kwa ukiri wetu.  Biblia inasema, “ Kwa hiyo, ndugu watakatifu, wenye kuushiriki mwito wa mbinguni, mtafakarini sana mtume na kuhani mkuu wa maungano yetu, Yesu,”(Waebrania 3 : 1).
Jinsi tunavyoongea duniani kama vile neno lisemavyo tuna ‘m-keep bize’ Yesu mbinguni.  Tunampa malighafi, yaani  maneno ya kuyafanyia kazi kama kuhani. Kukiri ni kusema kama Mungu asemavyo katika maandiko.  
Tunasema kama Neno lisemavyo,tunasema Yesu alitufanyia nini msalabani, alipofufuka na alipoketi mkono wa kuume.  Tunasema sisi ni nani kwake, yeye ni nani kwetu, tunasema tuna kitu gani ndani yake, tunasema kama Neno lisamavyo.  Imani ya Neno la Mungu huanzia mioyoni mwetu na utimilika vinywani mwetu. Imani hii iwapo kinywani kwa njia ya maneno tusemayo humwingiza Yesu kazini. Yesu amepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.  Anapata nafasi duniani kwa maneno yetu yaliyosawa na Neno lake.  Tunapotamka maneno haya, mamlaka ya utendaji wake hujidhihirisha. Biblia inasema, “Basi iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia  katika mbingu, Yesu mwana wa Mungu na tuyashike sana maungano yetu,” (Waebrania 4 :14). Tafsiri nyingine inasema, “Kwa kuwa tunaye Kuhani Mkuu kuliko wote ambaye ameingia mbinguni, Yesu Mwana wa Mungu, basi na tushikamane sana kwa uthabiti na ule ukiri wa imani yetu.  Tunaushika ukiri wetu, yaani maneno yetu yalisemalo Neno lake maana ameingia katika mbingu kwaajili yetu, ayahudumie maungano yetu.
Imani iliyopo moyoni husema kinywani.  Kile unachokijua kuhusu Mungu, kuhusu wewe katika Mungu au ushindi wako katika Kristo utakisema kwa kinywa chako, pia utakitarajia kudhihirika kwa kuwa unaye kuhani aliyesimama mbinguni kwaajili yako, ili adhihirishe maungano au maneno yako ya imani. Kama alivyosema ni lazima yatimizwe aliyoandikiwa (Luka 24:44), ni lazima ayatimize uliyoandikiwa wewe. Thubutu kusema kama neno lisemavyo katika moyo wako (Waebrania 13:5-6), atatimiza.








No comments:

Post a Comment