Malaika
ni Watumishi Wetu
Katika tafsiri ya Kiyunani neno malaika (angelos) lina maana sawa na mtumishi
aliyetumwa. Katika kitabu cha Waebrania imeandikwa maiaika ni roho waliotumwa
kuwahudumu wale watakaourithi wokovu (1:14). Watakaourithi wokovu ni kina nani?
Ni watu walio na Agano na Mungu kwa njia ya damu ya Yesu. Mtu yeyote aliyempa
Yesu maisha yake analo Agano na Mungu kwa damu ya Yesu. Amekuwa mrithi wa
Mungu. Malaika wapo ili wamuhudumie. Kama vile
watu wasioamini wanavyotegemea mapepo, majini na mizimu ili wafanikiwe, watu
wamwaminio Yesu inawapasa wamtegemee Mungu anayetumia malaika zake kuwahudumia.
Wanatumia
Neno la Mungu Kutumika
Malaika hutumia maneno kutenda. Jinsi
tunavyoongea ndivyo tunavyohudumiwa na malaika. Malaika wanasikiliza Neno la Mungu
na kulitenda (Zaburi 103:19). Wanafanya mapenzi ya Mungu ambayo ni Neno lake
(Zaburi 103:20). Roho wa Mungu anapokupa Neno na ukaanza kulisema unawaachilia
malaika walitende katika eneo au uhitaji husika . Unapotamka Jina la Yesu
wanaachiliwa pia, maana wapo chini ya jina hilo ni watumwa wa jina hili kuu. Wachawi na
waganga husema maneno mabaya na pepo huachiliwa kuyatenda. Wewe kama mtu wa
Mungu sema maneno mazuri
yaliyo
sawa na Neno la Mungu na malaika wenye nguvu zaidi ya pepo wataachiliwa.
I.Malaika
na Kazi au Biashara
Uzuri wa Mungu ni kibali chake kwetu.
Malaika wa Mungu wanaweza kutumika kuachilia kibali au uzuri wa Mungu katika maisha yetu na katika yale
tuyatendayo. Wanaweza kuleta kibali kwa wateja, waalimu au kwa mabosi kazini. Pepo
wanaharibu kibali, lakini kwa njia ya malaika kibali au uzuri wa Mungu unakuwa
juu yetu. Sema hivyo malaika watasikia na kutenda (Zaburi 103:17). Inakupasa
kuitamkia kazi, masomo au biashara yako kwamba inathibitika na kusimama,
Zaburi 90:17 inaonyesha hivyo. Unapofanya hivyo malaika wataachiliwa kwa
kusikiliza maneno yako katika Bwana na kuithibitisha kazi yako kwa nguvu za
Bwana.
II.Malaika
na Ulinzi
Biblia inasema Bwana atakulinda uingiapo na
utokapo, tena mabaya hayatatupata (Zaburi 121:8,91:10-11). Mabaya yoyote kama ni ajali, ujambazi, kupoteza viungo, kuumwa na nyoka
nk, katika Bwana hayatupati. Tunapokuwa na tabia ya kuyasema maandiko haya
malaika wa Bwana watakuwa kazini kuyatendea kazi na kutulinda. Watakusanyika
makundi makundi na kutulinda na mabaya ya aina zote, yakiwemo magonjwa, dumu
kusema hivyo usiseme mara moja au mbili (Zaburi
34:7).
III.Malika
na Adui Zetu
Watu wanaotuchukia na kututegea mitego,
malaika wanaitegua (Zaburi 35:5-8). Malaika wanafuatilia maadui zetu na
kuhakikisha kile walichotutegea kwa siri hakisimami, tutamke hivyo tutaachilia
malaika. Wanaponda watesi mfano wachawi na kupiga maadui mfano mapepo (Zaburi
89:20-23).
IV.Malaika
na Mahusiano
Katika mahusiano kwa mfano ya kuunganisha
mke na mume au kupata mchumba malaika wanahusika. Malaika alihusika kumsaidia
Yusufu asimwache Mariamu(Mathayo 1:20). Isaka alipata mke kwa njia ya mtumishi
wa Ibrahimu kuongozwa na malaika(Mwanzo 24:7). Unapotamka kwa jina la Yesu na
kusema malaika wanakusaidia kumpata mwenzi aliyekusudiwa bila shaka utaachilia
malaika wanaojenga mahusiano. Hata katika ndoa malaika wanahusika kusimamia
ndoa. Unaposema katika jina la Yesu mwenzi wangu hataniacha maana imeandikwa
mtu ataambatana na mume au mke malaika watatumia Neno hilo kuboresha ndoa yenu. Wachawi na washirikina
hutumia pepo kuharibu ndoa. Mungu hutumia malaika kuiboresha.
V.Malaika
na Watoto Wetu
Kuna malaika wanaosimama kwaajili ya watoto
wetu(Mathayo 18:10). Yesu alisema kuhusu watoto ufalme wa Mungu ni wao. Ufalme
ni haki, amani, furaha na mambo mengine ya Kiungu. Tunaweza kutamka kwa jina la
Yesu na kusema malaika wanaachiliwa katika tabia zao wawaongoze katika tabia za
kifalme. Pia tunaweza kuamuru mapepo yawaache waende kwa Yesu wakifundishwa na
malaika zake tabia njema badala ya kufundishwa na pepo. Usiombe malaika watende
hayo, tamka na kumwambia Mungu kwamba malaika wanatenda hayo. Hatuombi malaika
tunamwomba Mungu atumiaye malaika. Baada ya hapo tunatamka Neno na malaika
hulitenda.
VI.Malaika
na Majaribu
Wakati wa majaribu malaika wanakuwa karibu
nasi watutie nguvu. Yesu alipokuwa na majaribu malaika walikuwepo kumtia nguvu
(Marko 1:13). Wakati wa majaribu tujizoeze kusema Bwana ni nani kwetu; yeye ni
Mwokozi, ni ngome, ni kimbilio. Tumsifu kwa matendo yake makuu. Hali kama hii
itawaachilia malaika watutie Nguvu na kufungua milango kama
ilivyokuwa kwa Paulo na Sila (Matendo 16).
VII.Malaika
na Maombi
Kanisa linapoomba malaika huachiliwa. Kanisa
lilipomwomba Mungu kwaajili ya Petro malaika alitumwa na Mungu, Petro
akafunguliwa. Tunapokutana na vikwazo tuombe kwa bidii huku tukitumia Neno la
Mungu. Mungu atatuma malaika zake. Maombi mengi yanajibiwa kwa utendaji wa
malaika (Matendo 12:6-7).
VIII.Malaika
na Wokovu
Malaika wa Mungu wanashughulikia wagonjwa na
wasiookoka wakati wa huduma. Unapohudumu katika mkutano au semina na kuamuru
watu wapone na kuwasihi waokoke, malaika huwa pamoja na wewe. Mwinjilisti
Filipo katika huduma yake aliambatana na utumishi wa malaika (Matendo 8:26).
IX.Malaika
na Damu ya Yesu
Damu ya Yesu ni damu ya Agano. Inayo sauti
katika ulimwengu wa roho. Ukiona kuna jambo lolote limefanyiwa agano la damu
kwa mfano matambiko au uchawi. Tumia damu ya Yesu kubatilisha agano hilo. Damu itanena kazi
yote ya msalaba na ukombozi. Malaika watasimamia ushuhuda huo maana ni
watumishi na mashahidi wa kazi ya ukombozi ya Yesu. Kabla hajasulubiwa walikuwa
naye(Luka 22:43)alipofufuka walikuwepo(Luka 24:23) inawezekana hata
alipokomelewa misumari walikinga damu yake na
wanaifahamu.
X.Malaika
Hufunga Mashetani
Unapoamuru na kusema kwa jina laYesu pepo wa
udhaifu wa magonjwa au pepo yoyote katika anga afungwe. Malaika wa Mungu ndio
hufanya kazi ya kufunga ingawa ni wewe unayeamuru. Malaika wanafunga vitu
vibaya tunapoamuru na wanafungulia vitu vizuri tunapoamuru vitokee(Mathayo
18:19, Ufunuo 20:1-2).
Muhimu: Hakikisha umesoma
maandiko yote yaliyotajwa hapa. Kisha anza kuamuru utendaji wa malaika. Wewe ni
roho, unafanya kazi katika ulimwengu wa roho pamoja na malaika wa Mungu.
CFM PUBLISHERS
P.O.Box 15634
Arusha. Tanzania
Simu:0784535424
bmwakatundu@yahoo.com
|
No comments:
Post a Comment