Monday, March 2, 2015

Anajali!



Yesu Anajali
Bwana Yesu Kristo anajali hali uliyonayo. Hajabadilika, Kama alivyokuwa anajali hali za watu zamani ndivyo alivyo sasa, ni yule yule (Waebrania 13:8). Maandiko yafuatayo yanaonyesha NIA ya Yesu ilivyo kwetu, anatujali sana wanadamu, tunaona kujali kwake kwa namna alivyokuwa anaongea na watu kuitikia mahitaji yao.
I.  ANATUPA RIZIKI :  Mathayo 15:32, “Yesu akawaita wanafunzi wake akasema, Nawahurumia mkutano, kwa kuwa yapata siku tatu wamekaa pamoja nami, wala hawana kitu cha kula, tena kuwaaga wakifunga sipendi, wasije wakazimia njiani.” Unaona anavyosema Yesu hapa! Anasema kuwaaga makutano wakati hawajala HAPENDI. Hata sasa Yesu hapendi ukose chakula anajali hali yako ya kukosa riziki hapendi!
Yohana 21:5-6, “Basi Yesu akawaambi, Wanangu mnakitoweo? Wakamjibu La. Akawaambia litupeni jarife upande wa kuume wa chombo, nanyi mtapata. Basi wakatupa; wala sasa hawakuweza kulivuta tena kwasababu ya wingi wa samaki.  Unaona! Hapa pia Yesu alijali hali ya wanafunzi ya kukosa chakula. Akawaita WANANGU, Neno hili linaonyesha kujali, aliwaita wanafunzi wanawe! Akajali kutokuwa na kitoweo kwao kisha akafanya muujiza wakapata kitoweo.  Lilitakiwa jambo moja tu kwa wanafunzi, kutii kile walichoagizwa na Yesu, kutupa wavu upande mwingine. Yesu hajabadilika hata sasa, Tumsikilizapo atafanya muujiza tena, anatujali hata sasa.
II. HATAKI TUOGOPE: Mathayo 14:27, “Mara Yesu alinena, akawaambia, Jipeni moyo ni mimi msiogope”.  Wanafunzi walimwona  Yesu akitembea juu ya maji,  wakaogopa wakafikiri wanaona roho mbaya. Yesu akawaambia wasiogope ni yeye. Hapa tunaona akiwepo yeye, si wakati wa kuogopa. Yupo nasi wakati wote akituambia  tusiogope yeye yupo na sisi, anajali tusikiapo kuogopa, anatuondolea hofu kwa kuwa yupo nasi.
III. ANATAKA TUPATE RAHA: Mathayo 11:29, “Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mini ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu.  Yesu anataka tuwe tayari “kusarenda” kwake huku ni kujitia nira yake, pia  kujifunza jinsi alivyo, kisha kuishi kama yeye. Matokeo yake ni kupata raha nafsini mwetu. Yesu anapenda tupate raha ndani yetu, tujisikie vizuri. Kwa lugha nyingine ametupa amani yake, ametuachia amani yake, kisha akasema tusifadhaike wala tusiwe na woga. Ikiwa umefadhaika anajali hali yako hiyo, ndiyo maana amekupa amani yake, hapendi ufadhaishwe na chochote anataka imani yako iwe kwa Baba na yeye, yatoe macho yako kwa mazingira na kuiweka imani yako kwake ufanyapo hayo hutafadhaika (Yohana 14:27).
IV. ANATUANDALIA MAKAO:  “…Maana naenda kuwaandalia mahali…” (Yohana 14:2).  Anajali mwisho wetu mahali tunapoenda. Anasema amekwenda kutuandalia mahali. Kisha atarudi kutuchukua ili alipo tuwepo. Alipo katika heshima na utukufu anataka tuwepo; MBINGUNI!
USIKATAE KUJALI KWAKE. MPE MAISHA YAKO KWA KUSEMA “MUNGU NISAMEHE DHAMBI ZANGU YESU INGIA MOYONI, NIOSHE KWA DAMU YAKO”.  Kama umeshampa maisha yako usimwache, msifu, sema jinsi anavyokujali kwa kupitia maneno haya, utaona moyoni anavyokujali na kuwa na amani. Baada ya hapo utaanza kujali watu wengine kwa mfano wa Yesu anavyokujali wewe, UTAIVAA NIA YEKE.

No comments:

Post a Comment