Ngao
Ngao hukinga, Mungu wetu ni ngao
hutukinga na mashambulizi, alimwambia Abramu, “…Usiogope, Abramu mimi ni ngao yako, na thawabu yako kubwa sana.” (Mwanzo 15:1).
Imani katika Mungu hutukinga na maadui zetu, tunapomwamini kwa kuutumaini
uaminifu na upendo wake, yeye huwa ngao kwetu. Kumwamini kunaendana na yeye
kufanyika ngao, “Mungu wa mwamba wangu, nitamwamini yeye; Ngao yangu, na pembe ya wokovu wangu, mnara wangu, na makimbilio
yangu;” (2 Samweli 22:3). Tukiweka imani yetu kwa Mungu, tukimkiri na kumtegemea
anakuwa kinga yetu pande zote, “Na Wewe,
BWANA, U ngao yangu pande zote, Utukufu wangu na mwinua kichwa changu.”
(Zaburi 3:3).
Unataka Mungu awe kinga yako pande
zote? Mtegemee na kumsema hivyo, naye atakuwa hivyo kwako. Tumwaminipo Mungu,
nguvu yake huwa ngao kwetu na kutukinga na mashambulizi. Ngao ya imani ni nguvu
ya Mungu ambayo hutuzingira dhidi ya mashambulizi ya adui, tunapoziweka imani
zetu kwa Mungu.
Biblia inaonyesha kwa kusema, “Nanyi mnalindwa na nguvu za Mungu za Mungu
kwa njia ya imani hata mpate wokovu ulio tayari kufunuliwa wakati wa mwisho.”
(1 Petro 1:5). Maana mojawapo ya neno “mnalindwa”
katika andiko hili ni “mnakingwa”
kwa mfano wa kukingwa na ngao. Imani
zetu zikiwa thabiti kwa Mungu humpinga Shetani, huachilia nguvu ya Mungu ambayo
huwa ngao ya kumpinga Shetani, “Basi
mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye
atawakimbia.” (Yakobo 4:7), “Nanyi
mpingeni huyo, mkiwa thabiti katika imani,…” (1 Petro 5:9).
Katika Waefeso 6:16 maandiko
yanasema, “zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya
imani ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu,”
Hapa imani imetajwa kama silaha ikifananishwa
na ngao. Ngao hii imeonekana kuwa na uwezo wa kuzuia mishale ya moto ya
Shetani. Mishale hii bila shaka ni hila zote ambazo Shetani huzitumia katika
fikra au mawazo ili kumtoa mtu katika hali ya kuamini kwa kumtumaini Mungu
katika kudhihirisha alichosema. Wakati fulani nilikuwa katika jaribu, wazo
likanijia lisemalo “Mungu hakupendi
angekuwa anakupenda yasingekupata haya” Wazo hili lilikuwa kama mshale, moto wake ulikuwa hali ya mashaka na
wasiwasi kuhusu upendo wa Mungu kwangu. Niliweza kupinga wazo hilo
kwa imani katika pendo la Mungu kama maandiko
yanavyoonyesha, alinipenda na kumtoa Yesu kwaajili yangu ili nipate uzima
(1Yohana 4:9).
Hatutikisiki katika imani zetu kwa
Mungu kwa kuwa tunalijua pendo lake kwetu
na kuliamini, imani ya namna hii ni ngao kwetu kwa kuwa humfanya Mungu awe ngao
yetu pande zote kwa nguvu zake. Wazo lolote lililo na hofu ndani yake ni mfano
wa mshale wenye moto, lazima imani katika uaminifu
wa Mungu kwa yale aliyosema ilizuie, kwa kuachilia nguvu ya Mungu. Mshale
ni mfano wa wazo la kishetani, moto ni mfano wa woga au hofu inayokuja
na wazo hilo.
Ngao ya imani hufanya kazi kwa njia ya
kuamini uaminifu na upendo wa Mungu, Biblia inasema, “…uaminifu wake ni ngao na kigao” (Zaburi
91:4). Pia Biblia inasema, “Nasi
tumelifahamu pendo alilonalo Mungu kwetu sisi, na kuliamini…” (1Yohana
4:16). Shetani aletapo wazo kama mshale lisemalo, “ugonjwa huu utakuua” , imani
zetu hulipinga kama ngao kwa kuwa tunajua Mungu aliyesema kwa kupigwa kwa Yesu
tumepona ni mwaminifu na anatupenda
kiasi cha kudhihirisha uponyaji wake
kwetu, Wakati huo huo Mungu anakuwa ngao kwetu na kutukinga kwa imani zetu
kwake.
Maswali
1. Ngao hufanya
nini katika vita?
2. Fananisha utendaji wa ngao ya kawaida na imani
3. Kuna uhusiano gani kati ya uaminifu wa Mungu na ngao
ya imani
No comments:
Post a Comment