Jinsi Maagano Yalivyofanyika
Watu
walipokubaliana na kuapiana kuhusu jambo fulani kwa mfano kiapo cha kusema “yote yaliyo yangu ni yako na yaliyo yako ni
yangu”, au walipopeana ahadi, “sitakudhuru wala hutanidhuru. Baada ya kusema hivi walikata mnyama katikati
na wote wawili kupita kati yake. Baada ya kufanya hivyo walifungwa kwa vitu walivyoahidiana
au kuapiana, hii ilisababisha nguvu katika hayo waliokubaliana. Yoyote ambaye
angetangua makubaliano hayo ilimpasa afe au kupata laana. Mara nyingine laana
zilitamkwa kwa atakayevunja.
Mfano
wa agano lililofanyika kwa jinsi hii tunaliona katika andiko lifuatalo: “Na watu hao waliolivunja agano langu,
wasioyatimiza maneno ya agano lile, walilolifanya mbele zangu, wakati ule
walipomkata ndama vipande viwili wakapita katikati ya vipande vile.”
(Yeremia 34:18).
Katika
kitabu cha Mwanzo imeandikwa, “Akasema(Abramu), Ee Bwana Mungu, nipateje kujua ya kwamba
nitairithi? Akamwambia, unipatie ndama wa miaka mitatu, na mbuzi mke wa miaka
mitatu, na kondoo mume wa miaka mitatu, na hua, na mwana njiwa. Akampatia hao
wote, akawapasua vipande viwili, akaweka kila kipande kuelekea mwenzake…Ikawa,
jua lilipokuchwa likawa giza,
tazama , tanuru ya moshi na mwenge ulipita kati ya vile vipande vya nyama.”
(15:8-10,17). Hapa tunaona Mungu akimwapia Abramu kwamba atampa nchi ile. Mungu
alimwambia uzao wake watakuwa watumwa Misri lakini baadaye watairudia nchi ile.
Hiyo ilikuwa ni ahadi alisema
atalihukumu Taifa lile ambalo watawafanya watumwa, na baadaye uzao wake
utarejea nchi ile aliyomwahidi. Ili kuthibitisha kwamba atampa Abramu uzao kwa
wingi mfano wa nyota za mbinguni, na nchi ya uzao wake, Mungu alimwambia
ampatie wanyama awakate katikati na kisha Mungu mwenyewe akapita kati yao kwa mfano wa moto. Ni
agano aliloliandaa Yeye mwenyewe kwa kumwambia ampatie wale wanyama, kisha
baada ya Abramu kuwakata Mungu kulithibitisha kwa njia ya kupita katikati ya
wanyama, lilikuwa ni agano la “diatheke”.
Mungu
alijifunga kulitimiza na kumpa Abramu uhakika wa kuwa atapata uzao na nchi.
Abramu
akamwamini Mungu na kuhesabiwa haki kwa imani hiyo. Akaweka msingi wa watu watakaoamini
uzao wake uitwao Yesu Kristo kuhesabiwa haki kwa njia ya kumwamini Yesu na
Agano lake atakalofanya nao. Kwa hiyo wote
wamwaminio Yesu huitwa wana wa Ibrahimu kwa kuwa wanahesabiwa haki kama yeye. Mungu aliposema uzao wake utakuwa kama nyota alihusisha wote watakaokuja kumwamini Yesu
aliye Mzao, aletae wazao wengi waaminio. Wingi huo katika Kristo Yesu kwa wale
waaminio unaweza kuwa zaidi ya nyota. Mungu alipomwonyesha nyota zile alifanya
naye Agano la milele ambalo lilikuja kuhitimishwa katika Yesu Kristo na Kanisa
lenye Wayahudi na Mataifa wamwaminio Yesu, wote hawa ni wazao wa Ibrahimu katika
Mzao mmoja Yesu. Wote wawili katika imani zao kwa Yesu ni Kanisa moja.
Agano
la Mungu na Ibrahimu tunaliona kwa sura ya kuanzishwa kwa Kanisa la Agano jipya lenye Wayahudi na Mataifa wamwaminio Yesu,
waliofanywa mmoja katika Yesu (Waefeso 2:13-15).
Kwa
upande mwingine Agano hilo
lilionyesha kuanzishwa kwa Taifa la Mungu lenye mipaka ya Kijiografia liitwalo Israeli. Katika Israeli, Yesu alitokea
na katika Yesu Kanisa lilitokea. Kwa hiyo unapolitazama Agano la Mungu na
wanadamu kwa njia ya Yesu huwezi kuacha kutaja Israeli, Yesu, na Kanisa.
Kwa
nini Mungu alifanya Agano na Ibrahimu? Mungu alitaka kuanzisha UHUSIANO na
USHIRIKA na wanadamu kwa njia ya kujifunga nao kwa Agano. Alianzisha Agano ili
aweze kuandaa mpango wa kuhusiana na kushirikiana na wanadamu milele. Katika sura inayofuata tutaliangalia Agano
hili kati ya Mungu na Ibrahimu lililoonekana
na kuthibitishwa kutoka kwa Ibrahimu
mpaka Yesu na kutoka kwa Yesu kwenda kwa wanadamu wote waaminio kwa njia ya
injili. Injili inaleta Agano kwa wanadamu na kuwapa fursa kulikubali au
kulikataa.
Kwa
njia ya Adamu ushirika na Mungu ulivunjika kati yake na wanadamu. Ili aendelee
kushirikiana nao na kuwa na mahusiano nao na kukaa kati yao, Mungu alianzisha Agano kutoka kwa mmoja
yaani Ibrahimu.
Katika
Mwanzo 15, tumeona sehemu ya kiapo na
ahadi Mungu alizomwahidi Abramu. Hapa alitamka baadhi ya mambo yaliyopo kwenye
Agano lakini sio yote, aliyafunua kwa sehemu ingawa tayari alikata Agano na
Abramu kwa kupita kati ya wanyama. Abramu alipokuwa na umri wa miaka tisini na
tisa Mungu alimtokea tena na kuliweka wazi zaidi Agano lile lile.
Tutaenda
kusoma maeneo kadhaa katika Mwanzo 17:1-14). Baadhi ya maneno nimeyaandika
katika mabano kuonyesha Yesu, Israeli na Kanisa wameonekanaje katika Agano la
Mungu na Ibrahimu. Maandiko yanasema, “Abramu
alipokuwa mtu wa miaka tisini na kenda, Bwana akamtokea Abramu, akamwambia,
Mimi ni Mungu Mwenyenzi, uende mbele yangu, ukawe mkamilifu. Nami nitafanya
agano langu kati ya mimi na wewe, nami nitakuzidisha sana
sana. Abramu
akaanguka kifudifudi. Mungu akamwambia, akasema, Mimi agano langu nimelifanya
nawe , nawe utakuwa baba wa mataifa mengi(Kwa njia ya Yesu na Mataifa kumwamini, mataifa huwa watoto wa Ibrahimu
hapa agano hili linaonekana kuwahusisha wanadamu wote kwa njia ya Yesu aliyetoka
Israeli) wala jina lako hutaitwa tena
Abramu, lakini jina lako litakuwa Ibrahimu, kwani nimekuweka uwe baba wa
mataifa mengi.Nitakufanya uwe na uzao mwingi sana, nami ninakufanya kuwa
mataifa, na wafalme watokao kwako(kwa
njia ya Kristo). Agano langu
nitalifanya imara kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako, na vizazi
vyao, kuwa agano la milele, kwamba nitakuwa Mungu kwako na kwa uzao wako baada
yako.” Katika Wagalatia 3:16 kipengele hiki kinafafanuliwa hivi, “Basi ahadi zilinenwa kwa Ibrahimu na kwa
mzao wake. Hasemi, Kwa wazao, kana kwamba ni wengi, bali kana kwamba ni mmoja,
kwa mzao wako yaani Kristo.” Ukiendelea msitari wa saba wa Mwanzo 17
inasema, “Nami nitakupa wewe na uzao wako
baada yako nchi hii unayoikaa ugeni, nchi yote ya Kaanani, kuwa milki ya
milele, nami nitakuwa Mungu wao.” Hapa Mungu alikuwa akinena Agano lake katika
nchi atakayowapa Israeli kupitia Ibrahimu. Ukiendelea msitari kuanzia wa kumi
utaona Mungu alimwagiza Ibrahimu na uzao wake watahiriwe. Kutahiriwa ilikuwa ni
alama ya Agano walilonalo na Mungu. Katika agano Jipya alama hii ipo mioyoni
mwa waamini kwa njia ya kuzaliwa mara ya pili kwa uwezo wa Roho wa Mungu.
Katika
Mwanzo 22:17 kunakipengele kingine kinachoonyesha kwa upana zaidi Agano hili, kinasema uzao wa Ibrahimu utamiliki mlango wa adui, “katika kukubariki nitakubariki, na katika
kuzidisha nitauzidisha uzao wako, kama nyota za mbinguni, na kama mchanga
uliopo pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao.” Msitari wa kumi
na nane wa andiko hili katika Biblia iliyofafanuliwa unasema, “Na
kwa mzao wako[Kristo]mataifa yote ya dunia yatabarikiwa na[kwa Yeye]
watajibariki kwasababu umeisikia na kuitii sauti yangu.”
Baraka
hii aliyopewa Ibrahimu yaani Kristo iliachiliwa baada ya yeye Kristo, kufanyika
laana na kufa, kisha kufufuka na kuwaacha huru watu kutoka katika dhambi na
kuwapa kipawa cha Roho Mtakatifu, “Mungu,
akiisha kumfufua mtumishi wake Yesu, alimtuma kwenu ninyi kwanza, ili
kuwabarikia kwa kumwepusha kila mmoja wenu na maovu yake.” (Matendo 3:26).
“ Kristo alitukomboa katika laana ya
totati, kwa kuwa alifanywa laana kwaajili yetu; maana imeandikwa amelaaniwa
kila mtu aangikwaye juu ya mti, ili kwamba baraka ya Ibrahimu iwafikilie
Mataifa katika Yesu Kristo, mpate kupokea ahadi ya Roho kwa njia ya imani”
(Wagalatia 3:13-14). Baraka ya Ibrahimu imefika kwetu kupitia Kristo inaonekana
kwa sura mbili kubwa Wokovu na kipawa cha Roho Mtakatifu.
Kwa
ufupi agano lote alilofanya Mungu na Ibrahimu linahusisha mambo haya:
- Mungu kuwa wake na wa uzao wake.
- Mungu kuwapa wazao wake nchi.
- Ibrahimu kuwa baba wa Mataifa mengi.
- Kwa njia ya uzao wake mmoja(Kristo), mataifa yote watabarikiwa kwa kuachwa huru toka utumwa wa dhambi na kupokea kipawa cha Roho. Hili ni Agano la milele linalofungulia mlango wa Mungu kuishi na watu milele kwa njia ya imani zao kwa Kristo.
- Uzao wake kumiliki mlango wa adui.
Kwa jinsi tunavyoendelea
kujifunza utazidi kuelewa msingi wa mambo haya na nguvu yake katika maisha ya
mtu aliyeamini. Kumbuka kwamba huwezi kutaja Agano la ushirika wa Mungu na
wanadamu toka kwa Ibrahimu bila kutaja:Israeli, Yesu na Kanisa. Mambo haya
matano tuliyoyataja hapo juu yanahusika na Israeli, Yesu na Kanisa.
No comments:
Post a Comment