Sunday, August 3, 2014

Achilia Roho Njema


Kuachilia Roho Njema
Maneno hutenda kazi moja kwa moja na roho. Siwezi kuiona roho yako, lakini naweza kuiona unapoongea. Maandiko yanaonyesha maneno na roho hufanya kazi kama kitu kimoja. Katika Yohana 6:63, Yesu alisema maneno yake ni roho tena ni uzima. Mithali 18:21, inaonyesha mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi, mauti ni roho na uzima ni roho, zote hufanya kazi kwa ulimi. Ezekieli 2:2 inaonyesha Mungu aliposema na Ezekieli roho ikamwingia. Matendo ya Mitume 10:44, Petro aliposema Neno Roho aliwashukia waliomsikiliza. Yohana 20:22, Yesu aliwavuvia Roho wanafunzi kwa kusema neno.
Aina ya Roho na Hali ya Moyo
Hali ya moyo inaweza kuachilia aina ya roho fulani. Moyo wenye huzuni huachilia roho ya huzuni. Moyo wa woga huachilia roho ya woga. Moyo wa upendo huachilia roho ya upendo. Moyoni hutoka chemchemi nzuri au mbaya ambazo ni roho. Hutoka kwa njia ya maneno. Isaka, Moyo wake ulipofurahi aliachilia maneno ya baraka yenye roho ya baraka (Mwanzo 27:1-4, 27,28). Nuhu moyo wake ulipokasirika aliachilia maneno ya laana yenye roho ya laana (Mwanzo 9:24).
Maneno Yasemwapo Huendelea Kuwepo
Maneno yanapotamkwa hugeuka kuwa roho na kuendelea kuwepo, au huachilia roho inayotenda. Ukimsema mtu vibaya kwa moyo wa chuki au wivu, unakuwa unamzunguka kwa maneno hayo, kisha roho ya maneno hayo huanza kupigana naye. Maneno yanapigana kwa roho. Maandiko yanasema, “Naam, kwa maneno ya chuki wamenizunguka, wamepigana nami bure.” (Zaburi 109:3).
Ukiamua unaweza kumzunguka mtu na maneno mazuri au mabaya. Wakati wa maombezi ni muhimu kwanza usikie kumpenda mtu unayemwombea. Baada ya kusikia hivyo ukianza kuomba utaachilia maneno yanye roho njema itakayomzunguka na kuleta mambo mema.
Mara nyingine ukihisi kutamkiwa maneno mabaya, au ukiyasikia, tamka maneno mazuri kama Neno lisemavyo ili kuachilia roho njema. Ukiaa kimya maneno hayo yanaweza kukuzunguka na roho mbaya zikapigana nawe.

Jizungushie Roho Njema
Roho ya Ulinzi
Jizungushie roho ya ulinzi kwa kusema Bwana ni mwaminifu atakufanya imara na kukulinda na yule mwovu (2 Wathesalonike 3:3). Sema Bwana atakulinda na mabaya yote na kukuhifadhi mpaka utakapoingia mbinguni (2Timoteo 4:18).
Roho ya Ushindi
Katika hali zote sema unako kushinda kwa Yesu Kristo (1Wakorintho 15:57).Katika yote unashinda (Warumi 8:37).
Mara zote jizoeshe kuzungushia wengine roho njema kwa njia ya Neno la Mungu. Hii uifanye ukiwa na moyo wa furaha, amani na upendo. Utaleta hali ya hewa ya mbinguni kwako na wenzio.
Katika anga la Tanzania kuna manung’uniko mengi yanayoachilia roho mbaya. Ukisikia watu wanalalamikia kitu fulani juu ya nchi au Serikali, uwe karibu na Roho akuwezesha kuachilia roho njema katika mazingira hayo. Hii pia inaweza kufanyika kanisani, katika familia nk.

No comments:

Post a Comment