ANAJALI
Bwana Yesu Kristo anajali hali
uliyonayo. Hajabadilika, Kama alivyokuwa anajali hali za watu zamani ndivyo
alivyo sasa, ni yule yule (Waebrania 13:8). Maandiko yafuatayo yanaonyesha NIA
ya Yesu ilivyo kwetu, anatujali sana wanadamu, tunaona kujali kwake kwa namna
alivyokuwa anaongea na watu kuitikia mahitaji yao.
I. ANATUPA RIZIKI : Mathayo 15:32, “Yesu akawaita wanafunzi wake akasema, Nawahurumia mkutano, kwa kuwa
yapata siku tatu wamekaa pamoja nami, wala hawana kitu cha kula, tena kuwaaga
wakifunga sipendi, wasije wakazimia
njiani.” Unaona anavyosema Yesu hapa! Anasema kuwaaga makutano wakati
hawajala HAPENDI. Hata sasa Yesu hapendi ukose chakula anajali hali yako ya
kukosa riziki hapendi!
Yohana 21:5-6, “Basi Yesu akawaambi, Wanangu mnakitoweo? Wakamjibu
La. Akawaambia litupeni jarife upande wa kuume wa chombo, nanyi mtapata. Basi
wakatupa; wala sasa hawakuweza kulivuta tena kwasababu ya wingi wa samaki.”
Unaona! Hapa pia Yesu alijali hali ya
wanafunzi ya kukosa chakula. Akawaita WANANGU, Neno hili linaonyesha kujali,
aliwaita wanafunzi wanawe! Akajali kutokuwa na kitoweo kwao kisha akafanya
muujiza wakapata kitoweo. Lilitakiwa
jambo moja tu kwa wanafunzi, kutii kile walichoagizwa na Yesu, kutupa wavu
upande mwingine. Yesu hajabadilika hata sasa, Tumsikilizapo atafanya muujiza
tena, anatujali hata sasa.
II. HATAKI TUOGOPE: Mathayo 14:27, “Mara
Yesu alinena, akawaambia, Jipeni moyo ni mimi msiogope”. Wanafunzi walimwona Yesu akitembea juu ya maji, wakaogopa wakafikiri wanaona roho mbaya. Yesu
akawaambia wasiogope ni yeye. Hapa tunaona akiwepo yeye, si wakati wa kuogopa.
Yupo nasi wakati wote akituambia tusiogope yeye yupo na sisi, anajali tusikiapo
kuogopa, anatuondolea hofu kwa kuwa yupo nasi.
III. ANATAKA TUPATE RAHA: Mathayo 11:29, “Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mini ni mpole na
mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu.” Yesu anataka tuwe tayari “kusarenda” kwake huku
ni kujitia nira yake, pia kujifunza
jinsi alivyo, kisha kuishi kama yeye. Matokeo yake ni kupata raha nafsini
mwetu. Yesu anapenda tupate raha ndani yetu, tujisikie vizuri. Kwa lugha
nyingine ametupa amani yake, ametuachia amani yake, kisha akasema tusifadhaike
wala tusiwe na woga. Ikiwa umefadhaika anajali hali yako hiyo, ndiyo maana
amekupa amani yake, hapendi ufadhaishwe na chochote anataka imani yako iwe kwa
Baba na yeye, yatoe macho yako kwa mazingira na kuiweka imani yako kwake
ufanyapo hayo hutafadhaika (Yohana 14:27).
IV. ANATUANDALIA MAKAO: “…Maana naenda kuwaandalia mahali…” (Yohana 14:2). Anajali mwisho wetu mahali
tunapoenda. Anasema amekwenda kutuandalia mahali. Kisha atarudi kutuchukua ili
alipo tuwepo. Alipo katika heshima na utukufu anataka tuwepo; MBINGUNI!
USIKATAE KUJALI
KWAKE. MPE MAISHA YAKO KWA KUSEMA “MUNGU NISAMEHE DHAMBI ZANGU YESU INGIA
MOYONI, NIOSHE KWA DAMU YAKO”. Kama umeshampa
maisha yako usimwache, msifu, sema jinsi anavyokujali kwa kupitia maneno haya,
utaona moyoni anavyokujali na kuwa na amani. Baada ya hapo utaanza kujali watu
wengine kwa mfano wa Yesu anavyokujali wewe, UTAIVAA NIA YAKE.
No comments:
Post a Comment