Thursday, July 24, 2014

Amani Kiungo cha Kiroho






Bwana wa Amani
Amani ni ya muhimu ili tuweze kuomba kwa imani, kumsikia Mungu, kutoogopa pamoja na mambo mengine ya kiroho, ni kama kiungo cha kiroho. Maandiko yanasema, “Sasa Bwana wa amani awape amani daima kwa njia zote. Bwana na awe nanyi nyote.”
(2Wathesalonike 3:16). Katika andiko hili kuna maneno  ningependa kuyasisitiza nayo ni: daima na kwa njia zote. Biblia inaonyesha kwamba Bwana wa amani yaani Yesu anaweza kutupa amani daima na kwa njia mbalimbali. Amani hii itatuwezesha kuomba kwa imani bila woga.

Njia mojawapo ya kupata amani daima wakati wote ni toba. Tunapotubu dhambi tunapatanishwa na Mungu na kuwa na utulivu wa ndani yaani amani (Warumi 5:1). Baada ya hapo tutaweza kuomba kwa imani. Njia ya pili ya kupata amani daima ni Neno la Mungu. Neno linatupa kumjua Mungu, tunapoongezeka katika kumjua kwa ufunuo wa Neno lake tunazidi kuwa na amani. Omba Mungu alifunue Neno lake kwako kila unapolisoma ili umjue na kupata amani (Ayubu 22:21, Zaburi 119:165). Tatu amani huja kwa tunda la Roho Mtakatifu. Tunapompa nafasi Roho ayaongoze maisha yetu ni njia ya kuwa na amani daima. Anatuwezesha kuwa na amani ndani yetu na watu. Maombi ni njia nyingine ya kuwa na amani. Tunapoomba tunamkabidhi Bwana haja zetu, tunamtwisha fadhaa zetu. Baada ya kufanya hivyo tunatulia moyoni hatuhangaiki maana tunajua anashughulikia haja zetu (Wafilipi 4:7, 1Petro 5:7). Tunaweza kusema kama mwandishi wa Zaburi alivyosema, “Katika amani nitajilaza na kupata usingizi mara, maana wewe Bwana peke yako, Ndiwe unijaliaye kukaa salama.” (Zaburi 4:8). Damu ya Yesu ni chanzo cha amani kati yetu na Mungu. Kwa njia ya damu Mungu amekuwa rafiki yetu si adui tena (Wakolosai 1:20).

Paulo aliwatakia sana amani watu aliowatumikia. Bila shaka alijua ni kitu cha muhimu katika maisha yao ya kila siku, katika mahusiano yao na Mungu na watu.  Hata sasa unahitaji amani ya Mungu hasa katika fikra na mawazo yako ili uweze kuomba. Hii itakujengea ujasiri wa kiroho wa kuishi kwa imani na kumsikia Mungu akikuongoza kupitia amani. Mwongozo huu utakupa ujasiri wa kuomba. Katika maamuzi yote amani ya Mungu iamue au itawale katika moyo wako (Wakolosail 3:15).

Kama unapitia hali ya kukosa amani ambayo yakufanya usiweze kuomba;Dai amani ya Mungu kwa jina la Yesu, maana Yesu aliinunua kwaajili yako, amekupa amani yake (Yohana 14:13). Alikosa amani msalabani ili upate amani. Amani ikuwezeshayo kuwa na ujasiri mbele za Mungu hata uweze kuommba kwa imani, kumsikia Mungu, kutofadhaika na kutoogopa. AMANI YAKE IKUHIFADHI UTU WAKO WA NDANI.



No comments:

Post a Comment