Saturday, June 14, 2014

Haujui Ufanyeje Unapo pa Kutazama



Haujui Ufanyeje Unapo pa Kutazama
…Wala hatujui tufanyeje; ila macho yetu yanatazama kwako” (2 Nyakati 20:12)
Mfalme Yehoshafati alizungukwa na maadui.  Katika maombi yake kwa Mungu alimwambia, hajui afanyeje ila macho yake yalielekea kwake. INGAWA HAKUJUA AFANYEJE, ALIJUA ATAZAME WAPI.
Alikuwa napo pa kutazama, ingawa hakujua cha kufanya. Aliposema macho yetu yatazama KWAKO, neno hili kwako, linawakilisha nafsi ya Mungu. Katika agano jipya macho yetu yanatazama kwa Yesu. Yanatazama nafsi ya Yesu tu, katika hali zote zinazotuzunguka. Yeye alifanyika mwili akakaa kwetu, ni mfano wa Mungu asiyeonekana aliyeombwa na Yehoshafati.
Usomapo Injili: Yohana, Marko, Luka na Mathayo na ukakutana na maneno aliyosema Yesu yenye neno: mimi, langu, wangu, kwangu, au nami, maneno haya yanaonyesha nafsi ya Yesu ambayo yatupasa tuitazame hata kama hatujui tufanyeje, IWE NI SHABAHA TUSIIPOTEZE NA KUTAZAMA KITU KINGINE. Vita kuu ya ibilisi ni kututoa macho yetu kwake, macho yetu kuwa kwake ni wokovu kwetu.   Mifano ionyeshayo nafsi ya Yesu katika utendaji:
1. Mimi nilikuja ili wawe na uzima…(Yohana 10:10) 2. Njooni kwangu ninyi nyote…(Mathayo 11:28) 3. Kwa jina langu…(Marko 16:17) 4. Juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu (Mathayo 16:16-19) 5. Nami nawapa uzima wa milele wala hawatapotea… (Yohana 10:28). 6. …wala hana kitu kwangu (Yohana 14:30).
Katika hali yeyote uliyonayo itazame nafsi ya Yesu kwa maandiko kama haya yanavyoionyesha. Hata kama hujui ufanyeje. Katika asaya 45:22, Mungu anasema niangalieni mimi mkaokolewe. Yehoshafati alimwangalia Yeye akaokolewa.  Waebrania 12:2, inasema tukimtazama yeye aliyeanzisha na mwenye kutimiza imani yetu, yaani Yesu. Kwa kuwa yeye ni Mungu pamoja nasi (Mathayo 1:23), tumtazamapo tutaokolewa katika hali zote kama alivyosema katika Isaya 45:22.
Maandiko yanasema, “Kwa hiyo, ndugu watakatifu, wenye kuushiriki mwito wa mbinguni, mtafakarini sana mtume na kuhani mkuu wa maungamo yetu Yesu.” (Waebrania 3:1). Unaweza ukawa hujui ufanyeje, lakini unaye wa kumtafakari. Kutafakari ni kutazama kwa ndani.  Tafakari jinsi alivyokupenda. Jinsi alivyoondoa dhambi zako, jinsi alivyomshinda Shetani kwaajili yako, jinsi anavyokuandalia makao mbinguni, jinsi alivyoshinda magonjwa na mashetani kwaajili yako, alipokuwa duniani. Tafakari/mtazame yupo ndani yako, ikiwa umempokea! Hajabadilika yupo vile vile kama zamani (Matendo 13:8). Kama mashetani yalivyomwogopa (Marko 1:23-25), ndivyo yanavyomwogopa sasa akiwa ndani yako. Sema kwa  kinywa chako huku ukiitaja hali yako “Sijui nifanyeje, ninapo pa kutazama:
YESU AITWAYE KRISTO”

No comments:

Post a Comment