SEHEMU C:
I. UMUHIMU WA MEZA YA BWANA
Kuna mambo kadhaa ambayo yatupasa kuyajua au kuyafikiri na kuyasema tunaposhiriki meza ya Bwana.
UTII
1. Tunashiriki meza ya Bwana ili kumtii na kumuheshimu Yesu, maana ameagiza tuifanye kama wanafunzi wake, Tunamwonyesha utii wa moja kwa moja. Maana aliagiza kwa kusema tufanye hivyo kwa ukumbusho wake, “Akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa, akisema, Huu ndio mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu, fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu” (Luka 22:19).
AGANO
2. Agano kati ya Mungu na watu haliwezi kufanyika bila sadaka yenye mwili na damu. Meza ya Bwana ni alama kubwa ya muunganiko wetu na Mungu katika ushirika wetu na Yeye. Ushirika wetu na Mungu ni kwa kupitia mwili na damu ya Yesu, Mungu hukaa nasi kwa agano lake katika mwili na damu ya Yesu. Meza ya Bwana inachochea ufahamu huu, kutoshiriki meza ya Bwana mara kwa mara hutufanya tupoteze ufahamu wa muunganiko wetu na Mungu kiagano kwa mwili na damu, ulio juu ya agano lingine lolote katika ulimwengu wa roho. “kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi.” (Mathayo 26:28), “Kikombe nacho vivyo hivyo baada ya kula; akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu, inayomwagika kwa ajili yenu” (Luka 22:20).
UKUMBUSHO
3. Yesu alisema tufanye kwa ukumbusho wake. Wakati wa ushirika mtakatifu ni wakati wa kukumbuka kazi yote ya Yesu. Alifanyika dhambi kwa ajili yetu ili sisi tuwe haki kwa njia yake. Alimharibu Shetani msalabani kwa ajili yetu. Ni kuhani wetu tunaposhiriki meza ya Bwana yatupasa tufanye na maombi ya shukrani kwa kumkumbuka aliyetutendea mambo yote vema. Shetani hapendi kitu hiki ndio maana hatumaanishi kuhusu meza ya Bwana. Bila shaka kuna ngome zinatumika katika mawazo kutuzuia tusishiriki mara kwa mara au kabisa, “Akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa, akisema, Huu ndio mwili wangu unaotolewa kwaajili yenu, fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu” (Luka 22:19).
TANGAZO
4. Chakula cha Bwana ni tangazo la mauti ya Yesu hata ajapo, “Maana kila mwulapo mkate huu na kukinywea kikombe hiki, mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo” (1 Wakorintho 11:26). Kifo cha Yesu kilitoa damu ya ukombozi, ikiwa na maana ya kifo cha Yesu kimelipia kifo chetu kilicho tangazwa na torati. Yesu alipokufa alimharibu aliyekuwa na nguvu za mauti juu yetu. Kifo cha Yesu kimefunga agano la kale na kufungua jipya, ishara ilikuwa pazia la hekalu lilipasuka na njia ya kupaingia patakatifi pa patakatifu ikapatikana kwa mwili wa Yesu. Kifo cha Yesu kilimpeleka Yesu kuzimu na akatoka na funguo za mauti na za kuzimu. Kifo cha Yesu kimeleta kufufuka kwa Yesu, haya ni maisha mapya ya agano jipya. Kifo cha Yesu kimeua sheria ya Musa na kuleta imani ya Yesu. Haya yote tunayatangaza tunaposhiriki mwili na damu ya Yesu. Huwezi kuniambia sio muhimu kuyasema haya kwa njia ya kushiriki mwili na damu ya Yesu mara kwa mara. Bila kushiriki mwili na damu mara kwa mara kwa njia ya kuweka imani zetu katika yale Yesu aliyoyasema na kufanya msalabani, maisha ya kanisa yatakuwa ya kawaida. Kwa njia ya kushiriki kutakuwa na nguvu ya kuliendesha kanisa kiagano na kwa ushirika wa Roho Mtakatifu.
NJIA
5. Yesu alipochukua mkate aliumega, kwa lugha nyingine aliuvunja, aliuharibu. “naye akiisha kushukuru akaumega, akasema, Huu ndio mwili wangu ulio kwaajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu” (1 Wakorintho 11:24). Kuharibiwa kwa mwili wa Yesu ni njia pekee ya kumkaribia Mungu tuliyopata, “Basi, ndugu, kwa kuwa tuna ujasiri wa kupaingia patakatifu kwa damu ya Yesu njia ile aliyotuanzia iliyo mpya, iliyo hai, ipitayo katika pazia yaani mwili wake.”(Waebrania 10:19-20). Andiko hili linaonyesha damu na mwili wa Yesu kama njia ya kumkaribia Mungu. Tunamkaribia Mungu kwa damu kupitia mwili wake. Tafsiri ni hii, huwezi kumkaribia Mungu bila kuwa na damu, hapohapo huwezi kwenda na damu bila kupitia mwili wake. Unaposhiriki mwili wa Yesu, uliovunjwa msalabani kwa kutumia damu, unafika Mungu alipo na kupokea alivyonavyo, Pia kutoa ulivyonavyo na kumpa Yeye. Udhaifu ulionao unapeleka kwake, na nguvu alizo nazo anakupa wewe kwa njia ya mwili wa Kristo. Msalabani mwili wake ulikuwa dhaifu kama mwili wako. Alipofufuka mwili wake una nguvu ya kukutia nguvu mwili wako. Mwili wa Kristo ni njia ya kumkaribia Mungu na mabadilishano ya nguvu na udhaifu hutokea.
TUMAINI
6. Yesu alisema hatakunywa mzao wa mzabibu hata ajapo “Maana nawaambia ya kwamba tangu sasa sinywi mazao ya mzabibu hata ufalme wa Mungu utakapokuja” (Luka 22:18). Meza ya Bwana hutupa tumaini kwamba siku moja akirudi atatuchukua na tutaenda kula nae karamu ya Mwana kondoo mbinguni. Hii (meza ya Bwana) ni chombo kinachozishika imani zetu kumngojea. Tunajitakasa na kuishi kama wageni katika dunia hii tukijua siku moja tutamwona na kuishi naye milele. Meza ya Bwana ni chombo cha kumsubiria Yesu.
KWELI
7. Yesu alisema mwili wake ni chakula cha kweli na damu yake ni kinywaji cha kweli (Yohana 6:55). Mwili wa Yesu na damu yake ni chakula cha uhakika, ndani yake hamna uongo. Moja ya sifa kubwa ya Shetani ni baba wa uongo. Mwili na damu ni kweli, inayoonyesha nguvu juu ya uongo wowote wa kishetani katika maisha yetu, uliojificha au ulio wazi.
MUUNGANIKO
8. Kama vile ulapo chakula cha kawaida kinaunganika na maisha yako na kinaathiri mwili wako wote. Mwili na damu ya Yesu unatuunganisha na Yesu na tunayashiriki aliyonayo yanakuwa sehemu yetu, kwa Imani tayari tumeunganishwa na Yesu na kumshiriki, meza ya Bwana ni kichocheo cha kutukumbusha haya kiimani “Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu nami hukaa dhani yake. Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, nami ni hai kwa Baba, kadhalika nay eye mwenye kunila atakuwa hai kwa mimi” (Yohana 6:56-57). Uhai wa Yesu ndio uhai wa Mungu Baba, alipokuwa duniani walikuwa mmoja na ni mmoja hata sasa. Uhai wetu na Yesu ni mmoja kwa njia ya mwili na damu ya Yesu, uhai wa kanisa ni katika mwili na damu ya Yesu. Tunaposhiriki mara kwa mara na kusema hivyo, tutakuwa tunaziamsha imani zetu katika muunganiko na Kristo kati yetu wakati wote.
UFUFUO
9. Yesu anasema aulaye mwili wake na damu yake anao uzima wa milele naye atamfufua siku ya mwisho (Yohana 6: 54). Alama moja kubwa ya injili katika agano jipya ni ufufuo. Ipo siku watu wote watafufuliwa, katika ufufuo wa kwanza wa wenye haki na uufufuo wa pili wa wenye dhambi. Ufufuo wa kwanza ni wa wale walio na imani katika Yesu na kuokolewa. Meza ya Bwana inaonyesha kwa kumwamini Yesu kama Bwana na Mwokozi tuna uzima wa milele ndani yetu, na siku moja tutafufuliwa na Yeye katika uzima wa milele.
Meza ya Bwana sio mwili na damu ya Yesu halisi, ni alama ambayo inazifanya imani zetu zishike damu halisi na mwili halisi wa Yesu. Ili meza ya Bwana iwe na maana ni lazima, imani iwepo kwa kusikia neno la Kristo kuhusu mwili na damu yake. Tunaitenda kwa kumtii Bwana wetu Yesu , namna yoyote ya kuipuuzia ni kupuuza alichosema Yesu. Tukumbuke aliyesema ni Bwana wa mabwana na Mfalme wa wafalme, hivyo tumtii!
SHUKRANI
10. Ni vema meza ya Bwana iambatane na shukrani na maungamo ya imani kwa ukombozi. Kitu cha kwanza alichofanya Yesu alipouchukua mwili (Mkate) na kikombe (Damu) alishukuru, na kubariki “…Yesu alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa wanafunzi wake, akasema, Twaeni, mle; huu ndio mwili wangu.Akakitwa kikombe, akashukuru…”( Mathayo 26:26-27). Mwili na damu ya Yesu ni alama za shukrani mbele za Mungu, kwa ajili ya ukombozi wetu. Tunamshukuru mara kwa mara. Mara nyingi tunaomba sana Mungu atufanyie hili na lile. Namna ya kushukuru sana na vizuri ni kwa kutumia meza ya Bwana. Tunashukuru kwa yale aliyokwisha tufanyia, shukrani hizi zenyewe ni sadaka ni dhabihu (1Petro 2:9).
Kumbe! wakati wa kushiriki meza ya Bwana ni wakati wa kutoa dhabihu mbele za Mungu, yaani shukrani, Hapa ndipo jina la Eukaristi, lilipotokea, yaani shukrani.
KUFAHAMU
11. Yesu alipokuwa anamega mkate na kushukuru, ndipo macho ya wanafunzi wake yakafumbuka wakamfahamu “Ikawa alipokuwa ameketi nao chakulani, alitwaa mkate, akaubariki, akaumega, akawapa. Yakafumbuliwa macho yao, wakamtambua; kisha akatoweka mbele yao…Nao waliwapa habari ya mambo yale ya njiani, na jinsi alivyotambulikana nao katika kuumega mkate”(Luka 24:30-31,35). Yesu kabla mwili wake haujaharibiwa msalabani mlango wa wanafunzi kumfahamu ulikuwa umefungwa. Alipokufa na kufufuka Roho akaja, hapa ndipo ilikuwa chanzo halisi cha kuanza kumjua. Katika maandiko hayo tuliyoyasoma tunaona hali hiyo ya picha, alipomega mikate macho yao yakafumbuliwa wakamtambua. Meza ya Bwana ni alama ya kumjua Yesu kwa Roho ya ufahamu katika Roho Mtakatifu. Mara nyingine dai kuzidi kumfahamu Yesu kwa ufahamu wa rohoni, pale unapokula mkate yaani mwili wake.
SHEREHE
12. Yesu alipoanzisha meza ya Bwana ilikuwa ni kipindi sherehe ya pasaka na mikate isiyotiwa chachu (Kutoka 12). Pasaka ilikuwa sherehe ya kukumbuka ukombozi wa Israeli toka ufalme wa Misri. Meza ya Bwana ni sherehe ya kukumbuka ukombozi wetu toka ufalme wa giza hivyo kufurahi na kushukuru.