Thursday, October 1, 2015

Kumpokea Roho Mtakatifu 1

KATIKA SOMO HILI UTAPATA MSAADA WA KUWEZA KUJAZWA ROHO MTAKATIFU NA KUNENA KWA LUGHA.



I
KUJA KWA ROHO MTAKATIFU
Roho Mtakatifu ni Mungu, na ujio wake ulitabiriwa toka Agano la Kale. Ukaanza kuonekana kwa Kristo Yesu kama malimbuko, mwishoni ukadhihirika ndani ya kanisa lake ambalo ni mwili wake. Anaitwa ni Roho wa Ahadi, aliahidiwa.
ROHO NA YESU
Katika Agano la Kale maandiko yanasema, “Roho ya Bwana MUNGU i juu yangu; kwa sababu BWANA amenitia mafuta niwahubiri wanyenyekevu habari njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao. (2) Kutangaza mwaka wa BWANA uliokubaliwa, na siku ya kisasi cha Mungu wetu; kuwafariji wote waliao.” (Isaya 61:1-2)
Maandiko haya ya Isaya yalitimia Agano Jipya juu ya Yesu Kristo, alisema Yesu akinukuu maandiko haya, “Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa. (19) Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa” (Luka 4:18,21). Roho Mtakatifu anaonekana kupitia Yesu Kristo. Huwezi kumtaja Roho na kumpata Roho bila Yesu. Kuja kwa Roho Mtakatifu msingi wake ni kuja kwa Masihi yaani Yesu, na Roho huyo kuwa juu ya Yesu. Kila mtu atakaye kumpokea Roho lazima ajue anampokea tokea kwa Yesu.
DUNIA NA ROHO MTAKATIFU
Katika Agano la Kale kitabu cha Yoeli 2:28, maandiko yanaonyesha unabii wa Roho Mtakatifu kumwagwa duniani. Unabii huu ulitimia katika Matendo ya Mitume 2:1-4, imeandikwa, “(1) Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja. (2) Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kwa kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi. (3) Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. (4) Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka.” Maandiko katika mstari wa 16 – 21 wa sura hii na yanaendelea kuelezea unabii ule wa Yoeli 2:28-32.
Kipindi hiki tulichopo ni kipindi cha Roho Mtakatifu ameshamwagwa duniani ni kipindi cha kupokea Roho Mtakatifu aliyekwisha tolewa. Yoeli mlango wa pili ilikuwa inaonyesha unabii wa Roho Mtakatifu kuja, Matendo mlango wa pili inaonyesha kutimia kwa unabii huo kupitia Yesu Kristo.


No comments:

Post a Comment