KUISHI NA NENO LA MUNGU
(LOGOS na RHEMA)
I.
Lifahamu
Neno la Mungu. Katika maandiko, Neno la Mungu linaonekana kwa namna zifuatazo:
A.
Nafsi ya Mungu Mwana
Maandiko yanaonyesha Mwana
(Yesu) anaitwa Neno la Mungu. Ni Neno aliyefanyika mwili akakaa na watu (Yohana
1:1-5,14; Ufunuo 19:11-13).
B.
Sauti ya moja kwa moja ya Mungu kwa
mtu
Mungu huongea na watu
moja kwa moja kwa sauti ya wazi, sauti hii inaitwa “Neno la Mungu” aliongea hivyo
na Yohana mbatizaji (Luka 3:2).
C.
Matamshi ayatamkayo mtu kwa uwezo wa
Roho Mtakatifu
Roho Mtakatifu ana uwezo
wa kusema kupitia kinywa cha mwamini asemacho ni “Neno la Mungu” (1Timotheo
4:1,Luka 21:15,Matendo 6:10).
D.
Matamshi wayasemayo malaika toka kwa
Mungu
Mungu hutumia malaika
kuleta ujumbe kwa mtu, ujumbe huu huitwa “Neno la Mungu” (Luka 1:26-35)
E.
Maandiko-Biblia
Mungu hutumia maandiko
matakatifu, kusema na mtu Neno lake. Humtumia Roho wake Mtakatifu kusema nasi
kupitia maandiko. Maandiko(logos)+Roho
Mtakatifu=Neno la Mugu(rhema)
Sauti ya Mungu katika maeneo yote
manne yaliyotangulia, hupimwa au huthibitishwa na maandiko matakatifu katika
Roho Mtakatifu.Katika tafsiri ya Kiyunani Neno la Mungu limetafsiriwa katika
maneno makuu mawili 1.LOGOS na 2.REHEMA
LOGOS
Logos ni
wazo la Mungu la milele lisilofungwa na muda, wazo hili amelionyesha katika
maandiko. Maandiko ni wazo la Mungu (logos),
Soma Zaburi 119:89. Wazo hili limesimama mbinguni milele. Hakuna
kinachotokea duniani kiwezacho kulibadilisha mbinguni. Lilikuwepo, lipo na
litakuwepo. Wazo hili limeandikwa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kupitia mwanadamu
(1Petro 1:20-21). Ingawa maandiko au wazo la Mungu lipo wakati wote ni la milele; Ili kulitumia sasa Roho Mtakatifu hutoka katika
umilele na hulileta kwa watu binafsi wakati wa sas, kwa hitaji la sasa.
RHEMA
1. Rhema ni wazo la Mungu la milele laniloonyeshwa au
linalotumiwa sasa na Roho Mtakatifu.
Rhema ni Neno la Mungu la milele lisemalo sasa. Limekuja katika muda wa mtu sasa kwa hitaji
la sasa. Tofauti na logos, logos lipo siku zote katika umilele. Rhema huja sasa
kwa hitaji la sasa. Roho wa Mungu hulionyesha, hulifunua Neno la milele (logos)
katika maisha yetu ya sasa. Logos ni
ukweli wa milele wa Neno la Mungu katika maandiko. Rhema ni tafsiri
ya sasa ailetayo Roho katika hali yako ya binafsi kwa kutumia andiko.
2.Logos ni neno la Mungu kwa ujumla. Rhema ni neno la Mungu
maalum, litokalo katika Neno la jumla.
3.Logos ni neno la rohoni.
Rhema ni neno la nguvu ya kudhihirika mwilini.
4.Logos ni neno la nadhria, Rhema ni udhihirisho wa nadharia.
5.Logos ni maandiko yote, rhema ni maandiko unayoyahitaji
sasa, upewayo na Roho Mtakatifu.
6.Logos hukaa akilini Rhema hukaa moyoni, ni
andiko lililohuishwa na kuwekwa moyoni toka akilini na Roho Mtakatifu.
7.Logos hujenga matumaini
akilini , Rhema hujenga imani moyoni
UMUHIMU WA RHEMA
1. Ukitafakari na kusoma logos akilini,
Roho atakupa rhema moyoni
2. Yote yanawezekana kwa rhema (andiko
linaposema hakuna neno
lisilowezekana kwa Mungu, Luka 1:37, neno linalotajwa hapo kuwezekana ni
rhema).
3. Maandiko yanaposema imani huja kwa
kusikia (kuelewa-akouo) neno la Kristo neno hilo ni rhema (Warumi 10:17).
4. Usomapo Biblia na kuanza kuelewa
maandiko pasipo kufundishwa na mtu, kwa nanma hiyo utaanza kupokea rhema. Hili ni neno lililofunuliwa kwako, ni upako. Ukipata rhema umepata upako wa
kutimiza unachotakiwa kutimiza.
5. Rhema ni upanga wa Roho. Katika vita na mashindano Roho atakupa upanga
atalifunua neno na kuwa rhema kwako (Waefeso 6:12). Changamoto zinahitaji rhema.
6.
Yesu alisema imeandikwa (logos),
mtu hataishi kwa mkate tu, bali kwa kila neno
(rhema), litokalo katika kinywa cha Mungu (Mathayo 4.4). Rhema ni maandiko
yanayogeuka kuwa chakula kwako, sio maandiko tu. Ni maandiko yanayokufanya
uishi.
PIMA RHEMA KWA LOGOS
Waberoya walipata neno (rhema)
walilofundisha mitume, wakalipima kwa maandiko (logos), Matendo 17:11. Ufunuo
wowote uupatao katika maandiko au maono sasa, lazima uupime kwa maandiko yote
kwa ujumla au shauri na wazo la Mungu la milele (logos).
ISHI NA NENO
Wakati wote ishi na maandiko (logos)
kwa kuyasoma ili upate neno (rhema), hili ni andiko lililovuviwa na Roho kuwa chakula, upanga wa vita, mbegu ya
imani, nuru ya kukuongoza. Wakati
wote 1. Soma Biblia 2. Omba (hasa kwa lugha) 3.Tafakari (lirudie rudie akilini)
4. Uwe na moyo mwepesi 5. Sifu kwa kuimba 5. Andika mawazo mapya uyapatayo
katika maandiko (logos) au unapoomba, inawezekana mawazo hayo ni rhema. Kisha
yatumie katika maisha yako utaishi na Neno la Mungu. Utaishi na sauti ya Mungu.
Sauti ya Mungu ya uhakika huja kwa Neno lake (Logos na Rhema). Uanzapo kumsikiliza kwa jinsi hii utakuwa
salama.
No comments:
Post a Comment