Sunday, July 20, 2014

Yesu Bado Anatokea Watu-1

                   USHUHUDA WA MCH PAULO BUSUNGU



Roho Yangu Inatoka
Siku moja asubuhi kama saa kumi na mbili niliamka toka kitandani na kukaa. Nikasikia sauti ikisema nyuma yangu, “Leo unatoka duniani” Niliposikia sauti hii, ilinijia hali moyoni ya kujihurumia nafsi yangu na kusikitika masikitiko ambayo hayaelezeki.  Nilianza kububujikwa na machozi huku nikirudi kitandani.  Nilipolala tu, kitandani hazikupita hata dakika mbili nikatoka katika mwili wangu.  Nikajikuta nimesimama pembeni ya kitanda! Kitu cha ajabu nilikuwa nimesimama na hapo hapo najiona tena nimelala. Nilikuwa namwona ‘mimi’ mwingine amelala kitandani! Nilishangaa kujiona nimesimama wakati huo huo namwona mtu mwingine kama mimi kalala kitandani. Kumbe nilikuwa nimetoka katika mwili, nimekufa.  Niliyemwona mwingine kalala ni mwili wangu. Mimi halisi nilikuwa nimesimama.

Shimo  Lafunguka
Ghafla pembeni yangu kwa chini nikaona lango limefunguka, kumbe ni shimo refu sana lenyekutisha.  Niliona nisogee karibu na shimo hilo niweze kuona urefu wake.  Wakati ninasogea nilivutwa na nguvu ya ajabu ambayo siwezi kuielezea. Nilianza kuvutwa chini kama vile ninabembea huku nashangaa.  Nilifika chini sana, lakini haikuwa ni mwisho wa shimo. Ilikuwa niko mbali sana, nikagundua sikuwa ndani ya shimo nilikuwa ndani ya ulimwengu  mwingine!  Nikaanza kulia kilio ambacho sijawahi kulia.  Moyoni nilianza kupatwa na hali ya kuona nahitaji atokee mtu anisaidie.  Nilianza kukimbia kuelekea mashariki, huku nikilia kilio ambacho hakina maelezo. Nikawaza nikimbilie mashariki labda nitapata mtu wa kunisaidia.  Nilikuwa mwepesi mwenye kasi kubwa niliweza kuruka angani.  Chini yangu kulikuwa na mngurumo unaotisha. Nikapita kwenda magharibi, kusini na kaskazini. Nilipotoka kusini nilirudi huku nikikimbia kwa kukata tamaa, nilirudi mahali nilipoingilia huku nimekata tamaa ya kupata mtu wa kunisaidia. Nikaanza kulia sana kama muda wa nusu saa.


Ninaokolewa Toka Shimoni Kuzimu
Nikasikia wazo! Au sauti sijui! Ikisema moyoni mwangu, “angalia juu”.  Nikainua macho yangu juu, nikamwona mtu yupo juu sana ng’ambo nyingine.  Alinitazama kwa kunihurumia huku akinyosha mikono yake miwili kwangu.  Nilipoona mikono ile niliacha kulia na kuanza kujiandaa kumrukia ingawa alikuwa juu sana.  Moyoni niliazimia  lazima nimshike mikono na nikimshika nitamshika kwa nguvu kiasi kwamba ningeweza kurudi naye shimoni, ila asingeweza kuniachia.  Nikaruka nilikuwa mwepesi nikaenda juu mpaka alipo nikaingiza mikono yangu katika mikono yake.  Nilipoiingiza mikono akanipokea, akanichukua haraka na kuniweka mkono wake wa kuume.  Akaniangalia kwa sekunde! Sura yake sikuishika, akapotea.  Kisha yakatokea maandishi hewani pale alipokuwa amesimama, “YESU KRISTO”.  Hakuwa mwembamba wala mnene, alikuwa na kimo cha wastani.

Nimerudi Mwilini
Baada ya hapo nikajikuta nimeingia katika mwili wangu kitandani, nikakaa.  Ghafla nikasikia sauti nyuma yangu ikisema, “Wewe umetokaje huko, huko wakienda huwa hawatoki, wewe umetokaje? Sasa jiandae utarudi tena huko.” Niliijibu ile sauti na kusema kufa nakubali kufa, lakini kule shimoni sirudi nitaenda na Yesu.  Sauti ile iliendelea kunisumbua, ikasema tena, “Ulitokaje huko jiandae utarudi tena huko  Nikasema sitarudi tena huko naenda na Yesu, sauti ikanyamaza.

                                         

2 comments:

  1. Ni Amina na Kweli. Neema ya Kristo izidi Kutuwezesha Kumjua YEYE Aliye wa KWELI.

    ReplyDelete