Thursday, July 3, 2014

IWEKEE MPAKA HASIRA




Kudhibiti Hasira
Wote tuna hasira, hii ni nguvu iliyopo ndani yetu, Hata hivyo inapaswa idhibitiwe ili tusitende dhambi kwa hiyo. Hasira ipo kwetu ila yatupasa tuiweze.
“Vitu vyote ni halali kwangu, lakini si vyote vifaavyo; vitu vyote vi halali kwangu, lakini mimi sitatiwa chini ya uwezo wa kitu chochote.
(1Wakorintho 6:12)
1. Usikae na Vidonda
Shughulikia vidonda haraka, ulivyoumizwa, hasa vya wakati wa utoto. Mweleze Mungu jinsi ulivyoumia kisha mtwishe fadhaa hiyo kwa imani na kuacha kuibeba, mwachie yeye abebe uchungu au fadhaa hiyo. Ukidumu kufanya hivyo kwa muda utapona na hasira inayotokana na uchungu wa nyuma itaisha (1Pet 5:7).
2. Usiseme Mpaka Ufikiri
Jambo la kukasirisha, ambalo linaweza kukufanya upitilize kusema au kutenda, likitokea, usiseme chochote mpaka kwanza ujiweze kwa kufikiri (Yakobo 1:19).  Hasira huleta hali ya kutenda au kusema jambo bila kufikiri. Hivyo unapokasirika lazima ushike kufikiri kwako kusipote. Namna moja wapo ya kufanya ni kuondoka kwa muda eneo husika na kukaa sehemu tulivu huku mwili wako umetulia. Hii itakusaidia kufikiri kabla hujasema au kutenda jambo, pia itakuwezesha kujitenga na ugomvi (Mithali 20:3).
3.Omba Hekima
Hekima inaweza kuombwa kwa jina la Yesu (Yohana 16:23, Yakobo 1:15). Hekima ya Mungu inayo mambo mazuri, ina matunda mema (Yakobo 3:17). Ikaapo moyoni inaweza kukusaidia kufanya jambo jema la kudhibiti hasira, hekima inaweza kufanya jambo lolote jema ndani yako ikiwemo kutuliza hasira.
4. Jizuie Kuumiza
Mara nyingi moyo wa hasira hupenda kuumiza, Hasa kama chanzo cha hasira hiyo ni kuumizwa. Ukipenda kuumiza utaumia mwenyewe kwanza. Ukitaka kuumiza ukuta au hata mtu kwa kumpiga ngumi, maumivu yatatokea mkononi mwako kwanza! Kadhalika ukitamka neno baya la kuumiza unajiumiza mwenyewe kwanza. Ukifurahisha wengine utafurahi wewe kwanza. Huwezi shughulikia hasira ukiwa unaumiza watu! Haitaisha. Ukitenda mema kwa watu utaanza kupona wewe  kabla hata ya wao ! (Mathayo 7:12).
5. Vua Hasira
Unaweza kutenda lolote kwa jina la Yesu (Wakolosai 3:17). Unaweza kuivua roho ya hasira, hasira ambayo si ya kawaida inaweza kuwa ni roho, unaivua kwa jina la Yesu (Waefeso 4:23-24). Ivue katika hisia zako za nafsi kwa jina la Yesu.  Hasira iletayo dhambi waweza ivua kwa jina la Yesu. Ongea nayo kama roho.
6. Nena kwa Lugha
Ikiwa unanena kwa lugha tumia muda mrefu kunena.  Kunena kwa lugha kunakujenga katika mambo mbalimbali. Kunakufanya imara roho yako. Kunaweza kukusaidia kuidhibiti hasira. Ukasirikapo mara nyingine nenda mbele za Mungu, msifu na kunena kwa lugha, hisia mbaya za hasira zitaisha furaha itatokea!
HASIRA IPO IWEKEE MPAKA

1 comment:

  1. Thanks Pastor. Wengi tusaidika kwa hili pia. Bwana Azidi Kukutumia.

    ReplyDelete