Shukrani
Siku ya Jumamosi (12.7.2014),
nilipokuwa naongoza maombi kanisani nilisikia moyoni mwangu tufanye maombi
kwaajili ya kanisa zima kinyume na vifo vya ghafla. Siku iliyofuata, yaani jana usiku kama saa sita
hivi nilikuwa ninaomba na ghafla nikaanza kutamka kwamba Shetani hataniua.
Nilikuwa nikisema ninalindwa na
nguvu za Mungu kwasababu imani yangu ipo kwa Yesu (1Petro 1:13). Niliomba kwa kushindana na kutamka kwa
ujasiri. Pia niliendelea kutamka kwamba Yesu amekuja niwe na uzima (Yohana
10:10). Nilisema amekuja awe nuru ya ulimwengu, ili nisikae
gizani au katika ‘ushetani’ wowote (Yohana 12:46). Nilitamka na maandiko
mengine kadhaa. Baada ya hapo nilienda kulala.
Usiku nikaota naendesha gari
langu na nilipokuwa nazunguka “round about” nikagongwa nyuma mkono wa kulia na
gari ambalo sikuliona. Asubuhi, yaani
siku ya Jumatatu nilikuwa na safari ya kwenda Moshi kufuatilia shule ya mtoto
wangu. Nilipofika Kambi ya Mkaa, mbele kidogo ya Kikatiti, mbele yangu kulikuwa
na lori limeharibika na nusu yake liko barabarani, upande wangu wa kulia magari
yatokayo Moshi yalikuwa yanakuja, hivyo nafasi ilikuwa ndogo ya kuweza
kupita. Nilipunguza mwendo na nikapata
nafasi na kuanza kupita, nyuma yangu kulikuwa na basi linakuja, lakini halikuwa
karibu. Ghafla nilisikia mshindo mkubwa
upande wa nyuma ya gari kulia, basi lililokuwa nyuma lilishindwa kupunguza
mwendo, bahati!(neema), Nilikuwa nimeshalivuka lori lililokuwa limepaki
nikasogea kushoto, bila hivyo ningeweza kubanwa katika lori. Wakati huo huo kumbe basi hilo liliponigonga
liligonga na gari lingine mkono wa kulia lililokuwa limetokea Mererani. Wote
tuliogongwa ni wachungaji! Sitamtaja jina mwenzangu, Maana sikumtaarifu
nitaandika ushuhuda huu.
Leo jioni baada ya watu kufahamu
kwamba nimepata ajali, mtumishi wa Mungu mmoja anayenisaidia kuuza vitabu
akaniambia tokea jana alikuwa akiniangalia ananionea huruma na usiku aliniombea
kwa uchungu akishindana na roho ya mauti. Roho Mtakatifu alikuwa akifanya kazi
ya kuniokoa!
Kwa kweli Mungu ameniokoa! Ilikuwa
ajali mbaya itokee ambayo kibinadamu nisingeweza kuikwepa. Hatari kubwa mbili
zilikuwepo, gari liminywe kwenye lori au basi la nyuma linipandie. Mungu
ameniokoa na kifo cha ghafla.
Kwa Shukrani
Ninasema Maneno Haya:
BWANA ATANIOKOA NA KILA NENO BAYA NA KUNIHIFADHI HATA NITAKAPOFIKA
UFALME WAKE WA MBINGUNI (2 TIMOTEO 4:18).
NINALINDWA NA NGUVU ZA MUNGU KWA NJIA YA IMANI YANGU KWA YESU KRISTO
(1PETRO 1:5).
UHAI WANGU UMEFICHWA NDANI YA KRISTO YESU (WAKOLOSAI 3:3-4).
KAMA YESU ULIVYONIOKOA LEO UTANIOKOA SIKU ZOTE, NAKUOMBA UNAYESOMA
UMSHUKURU MUNGU PAMOJA NAMI.
No comments:
Post a Comment